KNEC yaonya kuhusu hatari ya wizi wa mitihani kurudi
Na WANDERI KAMAU
BARAZA la Kitaifa la Mitihani (KNEC) Jumatano limeonya kuhusu kuchipuka tena kwa mtandao mkubwa wa wizi wa mitihani unaohusisha baadhi ya maafisa wake, walimu, wazazi na wanafunzi.
Imebainika kwamba walimu wanaohusika katika njama hizo wamekuwa wakipokea pesa kutoka kwa wanafunzi kwa ahadi za kuwapa karatasi za mitihani ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) itakayofanywa katika miezi ya Oktoba na Novemba 2018.
Akiwasilisha ripoti kuhusu hali ya matayarisho ya mitihani Jumatano katika Taasisi ya Ukuzaji Mitaala Kenya (KICD) jijini Nairobi, Mwenyekiti wa baraza hilo Prof George Magoha alisema wako macho kuhakikisha kwamba wamesambaratisha mitandao hiyo.
Mwenyekiti huyo alisema kwamba wameanza mikakati ya kijasusi ambayo itahakikisha kwamba wale ambao wanahusika katika njama hizo wamenaswa na kukabiliwa kisheria.
“Tumefahamu kwamba kuna baadhi ya walimu ambao wanawaitisha wanafunzi pesa za kuwawezesha kupata karatasi za mitihani. Lakini tunawaambia kwamba tuko macho. Uchunguzi wetu umebaini kwamba baadhi wanaitisha hadi Sh20,000,” akasema Prof Magoha.
Alisema kuwa wameimarisha juhudi zao katika usimamizi wa mitihani hiyo, kwa kuongeza maafisa wa usalama na mitambo ya teknolojia.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuhakikisha kwamba walimu wakuu lazima wawepo katika ufunguzi wa kontena za mitihani. Walimu hao pia lazima wahakikishe kwamba hakuna mtu asiyetakikana anayekuwa karibu na mazingira ya kituo husika wakati mitihani hiyo inaendelea.
Kwa sasa, walimu 60 wanaendelea kuchunguzwa kwa tuhuma za kushiriki katika wizi huo mwaka uliopita.
Kwa muda wa miaka miwili iliyopita, KNEC kwa ushirikiano na idara nyingine za serikali ilifanikiwa kupunguza udanganyifu kwenye mtihani, hatua ambayo imefurahiwa na Wakenya wengi.
Wizara ya Elimu pia imeonya kwamba shule ambazo zitapatikaba kuhusika katika aina yoyote ya udanganyifu zitafungwa mara moja.
Akihutubu katika taasisi hiyo, Waziri wa Elimu Amina Mohamed alisema kwamba hiyo ndiyo itakuwa hatua pekee ya kuhakikisha kwamba wanaopaswa kusimamia mitihani hiyo wamewajibika ifaavyo
“Hatutaketi kitako kuona watu wachache wakiwaharibia watoto wetu maisha ya baadaye. Tutafunga shule hizo ili kutotumika tena kama jukwaa la kuendeleza udanganyifu,” akaonya waziri.
Mwaka uliopita, matokeo ya wanafunzi 1,200 yalifutiliwa mbali na baraza hilo baada ya kubainika kwamba walishiriki katika udanganyifu.
Mwaka huu, jumla ya wanafunzi 1,060,703 wamejisajilisha kufanya mtihani wa KCPE, huku wanafunzi 664,585 wakisajiliwa kufanya ule wa KCSE.
Kulingana na KNEC, hilo linaashiria ongezeko la wanafunzi zaidi, ikizingatiwa kwamba mnamo 2017, watahiniwa 1,002,922 waliufanya mtihani wa KCPE, huku 577,253 wakifanya mtihani wa KCSE.
Wizara pia iliahidi kufanya ukarabati wa shule ambazo ziliharibiwa na mafuriko na zitatumika kama vituo vya kufanyia mitihani, ili kuhakikisha kwamba hakuna wanafunzi ambao wanakosa nafasi ya kuufanya.