Habari Mseto

'Kusomea nyumbani si rahisi'

June 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na DIANA MUTHEU

WANAFUNZI wengi wa vyuo vikuu wamelalamika kuwa kusomea nyumbani kuna changamoto nyingi sana.

Akizungumza na Taifa Leo, Kelvin Mumo ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Mombasa (TUM) alisema kuwa wanapata changamoto kutumia wavuti.

“Wengine wetu hatuna simu za kidijitali, kompyuta, nyumbani hakuna stima na pia lazima tusaidie wazazi wetu kufanya kazi za nyumbani ambapo kwa wakati mwingine huchukua muda mrefu,” akasema Mumo.

Brian Atieno ambaye ni mwanafunzi wa chuo kingine jijini Mombasa alilalamika kuwa baadhi ya masomo yanakumbwa na uzito mwingi hasa kama yanahitaji uamilifu wa hali ya juu ambapo wanafunzi wanafaa kutengeneza, kufanya, na kuunda vitu halisi na utendaji (practicals).

“Nasomea udaktari na mara nyingi huwa tunafanya masomo katika maabara shuleni. Hatuna vifaa na sampuli muhimu nyumbani na tumelazimika kusoma tu madaftari tukisubiri shule zifunguliwe tuingie katika maabara hayo,” akasema Atieno.

Akigusia swala hilo, Naibu Chansela wa TUM, Prof Laila Abubakar alisema kuwa changamoto kama hizo zipo kwa kuwa asilimia 30 tu ya wanafunzi walikuwa wamezoea kusomea kozi zao mtandaoni.

“Masomo yanaendelea mtandaoni na tumejadiliana na wahadhiri kuwa pia watume mafunzo hayo katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp, baruapepe na hata katika njia ya SMS ili kila mwanafunzi aweze kusoma,” akasema Prof Abubakar.

Naibu Chansela huyo alisema kuwa ana matumaini kuwa vyuo vitafunguliwa ifikapo Septemba.

“Hata hivyo, tutahakikisha kuwa wanafunzi ambao wako katika mwaka wao wa mwisho na wale wapya chuoni ndio tutawasajili,” akasema.