LEUSHADORN LUBANGA: Afichua kutamaushwa na waigizaji wa Citizen TV kumtaka kingono kwanza
Na JOHN KIMWERE
ANAPENDA kuigiza lakini anawaponda baadhi ya wasanii waliowatangulia ambao hupenda kuwashusha wenzao kwa kuwataka kingono ili kuwapa ajira.
Mwigizaji anayeibuka Leushadorn Lubanga, anasema tayari amekosa imani baada ya kupewa sharti hilo ili kupata nafasi ya kuigiza kwenye filamu za kipindi ambacho hupeperushwa kwenye runinga ya Citizen TV.
”Bila kupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa wapo wanaume wawili waigizaji kwenye kipindi hicho kilicho maarufu kwa wapenzi wa tasnia ya filamu nchini ambao baada ya kukutana nao walinieleza peupe kuwa mwanzo wa ngoma tufanye mapenzi mara moja,” anasema na kuongeza kwamba bosi wa kipindi hicho humpigia simu mara kwa mara na kumweleza kuwa nafasi ya ajira ipo lakini hadi atakapokubali matakwa yao.
Aidha anasema kisa hicho kimemfanya kuhofia zaidi kusaka ajira kwingine na sasa hawezi kukutana na mwanaume asiyefahamu. Licha ya hayo anasema ana imani ipo siku azma yake itakapotimia na kuona akivuna matunda ya uigizaji.
Anaitaka serikali ya kitaifa kutambua sekta ya filamu maana wapo wengi waliotuzwa talanta ya uigizaji lakini hakuna pa kufanya kazi.
”Serikali inastahili kusapoti tasnia ya filamu ili kusaidia wengi kujiepusha dhidi ya matendo maovu kama wizi na mengineyo,” alisema na kudai taifa hili limejaa waigizaji wengi ambao wakipata sapoti watavumisha sekta ya filamu kufikia mataifa mengine barani Afrika ikiwamo Nigeria na Tanzania.
Ingawa hajakomaa katika sanaa ya uigizaji anasema ameazimia kujituma kisabuni kuhakikisha amefikia kiwango cha mwigizaji Sarah Atieno maarufu kama Lavender ambaye hushiriki kipindi cha Inspetka Mwala ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV.
Dada huyu aliyezaliwa eneo la Marenyo, Butere Kaunti ya Kakamega anasema kimataifa anatamani sana kutinga kiwango chake mwigizaji wa Tanzania Wema Sepetu. Anadai wawili hao hufanya kazi zao kwa kujituma pia kujiaminia.
Kadogo anajivunia kushiriki filamu iliyofahamika kama ‘One in a Millioni’ ambayo haikufanikiwa kupeperushwa popote.
Kadhalika alishiriki filamu iliyotegenezwa na kundi la Ramba Prodution iliyoitwa Ramba Ramba, produsa wake akiwa Clement Wesonga. Kwenye filamu hiyo alishiriki kama mtoto wa bosi yaani landilodi aliyetwaa jukumu la kuchunga wapangaji ambao hupenda kusepa bila kulipa kodi ya nyumba.
Kadogo alivutiwa na uigizaji akisoma darasa la nne kwenye shule ya Marenyo, Butere. Anasema mamake aliyekuwa akipiga hatua yake hatimaye ameshafahamu kwamba uigizaji ni ajira kama nyingine.
Hata hivyo anasisitiza kwamba angependa kujiongezea maarifa zaidi kuhusu uigizaji. ”Nimetambua kwamba ili kufikia viwango vya kimataifa inahitaji maarifa zaidi,” alisema.
Kadhalika anazitaka kampuni zinazomiliki vituo vya televisheni kuzipatia filamu za nyumbani nafasi kubwa kuliko muvi za mataifa za nje.
Anasema waigizaji walitangulia hawana budi kukomaa na kuwaheshimu wadogo wao wanaokuja. Anadai wanastahili kufahamu wapo kwa muda tu maana ndiyo watakaoshika usukani pale wao watakapostaafu.