Maafisa 4 ndani miaka 3 kwa wizi na kutumia afisi kujinufaisha
Na RICHARD MUNGUTI
ALIYEKUWA Katibu wa Wizara ya Serikali za Wilaya, Sammy Kirui pamoja na maafisa wengine watatu wakuu wa baraza la jiji NCC Jumanne walisukumwa jela miaka mitatu na kupigwa faini ya Sh86 milioni.
Bw Kirui, aliyekuwa katibu mkuu wa NCC John Gakuo, katibu wa masuala ya sheria Mary Ng’ethe na mwanakamati wa kamati ya zabuni Alexander Musee wanajiunga na orodha ya waliokuwa maafisa wakuu wa serikali kusukumwa jela makatibu Sylvester Mwalikho na Rebecca Nabutola waliofungwa kwa ufisadi.
Wanne hao walipatikana na hatia ya kujihusisha na utowekaji wa Sh283milioni katika kashfa ya kununua ardhi ya kuwazika wafu katika eneo la Athi River kaunti ya Machakos miaka 10 iliyopita.
Mbali na kifungo hicho cha jela wanne waliofungwa walitozwa faini kati ya Sh1milioni hadi Sh52milioni.
Hakimu Douglas Ogoti aliyewapata na hatia Mabw Kirui, Bw Gakuo, Bi Mary Ng’ethe na mwanakamati Bw Alexander Museee alisema “upande wa mashtaka umethibitisha wanne hao walitumia vibaya mamlaka ya afisi zao na kupelekea Serikali kupoteza zaidi Sh283milioni.”
Bw Ogoti aliwatoza Mabw Kirui na Gakuo faini ya Sh1milioni kila mmoja pamoja na kifungo cha miaka mitatu.
Naye Bi Ng’ethe alitozwa faini ya Sh52milioni ilhali Bw Musee alitozwa faini ya Sh32milioni.
Akipitisha hukumu aliyosoma zaidi ya masaa mawili , Bw Ogoti alisema washtakiwa walikaidi mwongozo wa ununuzi wa mali ya umma na kuidhinisha ardhi hiyo inunuliwe katika eneo ambalo halikufaa kwa makaburi.
Ardhi hiyo ilinunuliwa kati ya Desemba 2008 na Aprili 2009.
“Mabw Kirui na Gakuo walikaidi ushauri wa wataalamu wa masuala ya ununuzi wa ardhi waliosema ardhi hiyo haikufaa kwa kuwazika wafu lakini wakaamuru ununuzi uendelee,” alisema Bw Ogoti.
Mahakama ilisema washtakiwa wanne hao walipuuza sheria na mwongozo uliowekwa na kuruhusu mamilioni ya pesa za umma zitumiwe kwa njia isiyofaa.
Bw Kirui alikuwa katibu mkuu wa Wizara ya Serikali za Wilaya ilhali Bw Gakuo alikuwa Katibu mkuu wa baraza la jiji la Nairobi wakati wizi huo ulitekelezwa.
“Maafisa hawa walikuwa na uwezo wa kuzuia pesa hizi kutotoweka lakini walitumia vibaya mamlaka yao,” alisema Bw Ogoti.
Mahakama ilisema kuwa mashahidi waliofika kortini walieleza jinsi walikuwa wanakopeshwa pesa hadi kiwango Sh18milioni na baadhi ya washtakiwa.
“Pesa hizi zilipopelekwa City Hall ziligawanwa na maafisa wakuu waliokaidi ushauri kuwa ardhi hiyo haikufaa kwa kuwazika wafu kwa vile ilikuwa na mawe mengi,” alisema Bw Ogoti.
Ardhi hiyo ilikuwa itumike na baraza la jiji la Nairobi kuwapeleka maiti kuwazika katika kaunti ya Machakos.
Wanne hawa walikuwa miongoni mwa washtakiwa 15 walioshtakiwa kwa kashfa hiyo ya makaburi.
Wengine waliofikishwa kortini ni pamoja na aliyekuwa Meya Geoffrey Majiwa (aliyeachiliwa kwa kukosekana ushahidi) , Mabw Maina Chege, Naen Rech Limited, Newton Osiemo, Wakili Alphonce Mutinda, Nelson Otido, Joseph Kojwando, Alexander Musee, Daniel Nguku, Herman Chavera, William Mayaka na mawakili Paul Chapia Onduso na Davies Odero.
Maafisa wengine wa serikali waliofungwa awali kwa ufisadi ni waliokuwa makatibu Sylvester Mwaliko miaka mitatu kwa kashfa ya Anglo-Leasing na Bi Rebecca Nabutola.