Madereva kutoka Kenya wadai wanawekwa katika vituo duni vya karantini Uganda
Na WINNIE ATIENO
WAWEKEZAJI katika sekta ya uchukuzi nchini wameishtumu serikali kwa kushindwa kuwalinda dhidi ya changamoto ambazo madereva wa masafa marefu wanakabiliana nazo wanaposafirisha mizigo hadi nchini Uganda.
Wamesema madereva wamekuwa wakihangaika kila wanapoingia Uganda ikizingatiwa tahadhari kuu iliyoko ya kujaribu kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.
Wawekezaji hao sasa wanaitaka serikali iingilie kati swala hilo ili madereva wao wasiwekwe katika vituo duni vya karantini ambavyo “haviambatani na kanuni za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).
Kupitia afisa mkuu wa muungano wa madereva wa masafa marefu nchini, Bw Denis Ombok, wawekezaji hao walidai sehemu za kuwaweka kwenye karantini nchini Uganda ambapo baadhi walipatikana na virusi vya corona ziko katika hali mbaya.
“Kuna uwezekano wa wale ambao wanaendelea kuwekwa kwenye vituo hivyo waambukizwe maradhi mengine kando na Covid-19. Kwanza mazingira na usafi wa sehemu hizo ni duni, hasa vyoo ambavyo viko katika hali mbaya zaidi,” amesema Bw Ombok akizungumza Jumapili mjini Mombasa.
Bw Ombok alisema inasikitisha kwamba madereva wa humu nchini wanaendelea kupatikana na virusi hivyo wanapofika maeneo ya mipakani.
Amedai kuwa baadhi ya madereva hao wamelazimishwa kusafisha sehemu hizo.
“Sehemu za karantini nchini Uganda hazifai kuwekwa mwanadamu; madereva wetu wana msongo wa mawazo na pia wanahangaishwa kwenye vizuizi huko Uganda na pia kunyanyapaliwa,” ameongeza.