Habari Mseto

Madiwani, Maalim wapinga ‘Shirika Plan’ Garissa

Na KEVIN CHERUIYOT March 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MADIWANI kutoka Bunge la Kaunti ya Garissa wamepinga vikali mipango ya serikali ya kuwashirikisha wakimbizi kutoka kambi ya Dadaab kama sehemu ya jamii ya eneo hilo.

Serikali ikishirikiana na Shirika la Kitaifa kuhusu Wakimbizi (UNHCR) na mashirika mengine ya maendeleo, inatarajiwa kuzindua mpango wa kuwashirikisha wakimbizi katika jamii maarufu kama ‘Shirika Plan

Suala hilo limewafanya madiwani wajikune kichwa wakiwa na hofu kuwa usalama wa jamii zao utahatarishwa na sasa wanalipinga.

Diwani wa Labisagale Mohamed Sheikh aliwaongoza wenzake kupinga mpango huo wanaosema wamepata mwao, utazinduliwa na Rais William  Ruto hivi karibuni.

“Tunamwomba Rais Ruto aahirishe uzinduzi huu au hata kuutupilia mbali ili azungumze nasi,  asikie malalamishi yetu na ayatilie manani,” Bw Sheikh akasema kwenye taarifa akiwa jijini Nairobi.

Kwa kuwa idadi ya wakimbizi ni maelfu, viongozi hao wanadai visa vya utovu wa usalama na hata ugaidi vinaweza kutokea na kusambaratisha maisha ya jamii asili.

“Hatuelewi kwa nini mpango huu unaharakishwa. Kama kuna wafadhili ambao wanashinikiza serikali, tungependa kuwaambia watafute njia nyingine au wawarejeshe wakimbizi hawa makwao,” akaongeza Bw Sheikh.

“Hatuwezi kukubali mpango huo ulazimishiwe raia kwa sababu athari zake nazo zitakuwa hasi na haki zao zitakuwa zikikiukwa. Hatua ya serikali kuwatelekeza washikadau, kutotilia manani malalamishi na kuharakisha mpango huo kutaleta tu ghasia na kunazua shaka,’

Diwani huyo sasa anasema kuwa kama Rais atazindua mpango huo,  rasilimali chache zitang’anganiwa na wakazi wa Kaskazini Mashariki hata watalemewa kunufaikia huduma muhimu wanayofurahia kwa sasa.

“Jamii yetu itakuwa ikipata nini?  Wakimbizi je? Kutekeleza mpango huu hautakuwa rahisi jinsi ambavyo wanafikiria,” akasema.

Aidha walidai mpango huo wa kuwashirikisha wakimbizi wa Dadaab katika jamii unasukwa Nairobi, hali ambayo inabua shaka zaidi.

Pingamizi za madiwani hao zimeungwa mkono na Mbunge wa Daadab Farah Maalim ambaye alisema wengi wa wakimbizi wangetaka kurejea Somalia na wasaidiwe wakiwa huko.

“Serikali ya Somalia iko tayari kuwapokea wakimbizi hao mradi tu kuwe na msaada kutoka kwa mashirika. Magavana wa maeneo ambayo wakimbizi wapo hawafai kuongozwa na tamaa ya kunufaikia hela za mashirika ya kusaidia wakimbizi,” akaandika Bw Maalim mtandaoni.

“Viongozi wote wa Garissa wanapinga mpango huo isipokuwa Gavana Nathif Jama. Hata Waziri Murkomen (waziri wa usalama wa ndani) tumemwaambia hivyo,”

Kambi za wakimbizi za Daadab na Kakuma zina wakimbizi zaidi ya 800,000 ambao viongozi wanahofia wakishirikishwa katika jamii, basi kutakuwa na janga la kibinadamu.