Madiwani wapata uungwaji wa mswada wa kuwatengea pesa za maendeleo
MASENETA wanashinikiza mabunge ya kaunti yapatiwe uhuru wa kifedha, hatua inayolenga kuwapa wawakilishi wa wadi uhuru kutoka kwa magavana.
Haya yanajiri huku maseneta wakiunga mkono Mswadau unaotaka kuhakikisha uhuru wa kifedha wa mabunge ya kaunti yanapoendesha shughuli zao.
Mswada huo – Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Fedha za Umma wa Kaunti, 2023 – umefadhiliwa na Seneta wa Meru Kathuri Murungi.
Seneta huyo alieleza kuwa Mswada huo, ulio katika hatua ya pili ya kusomwa katika Seneti, unalenga kurekebisha sheria za fedha za umma ili mabunge ya kaunti yapate pesa zao moja kwa moja kutoka kwa Hazina ya Kitaifa.
Zaidi ya hayo, unapendekeza kuundwa kwa Hazina ya Bunge la Kaunti ambapo karani wa bunge atakuwa msimamizi.
Kwa sasa, alisema, mabunge ya kaunti yanapotaka kuomba pesa, hupitia Mawaziri wa Fedha wa kaunti zao.
“Madiwani wanapotaka pesa ili wafanye kazi yao ya usimamizi na kutayarisha mipango yao, lazima waende na kupiga magoti kwa waziri wa fedha wa kaunti ambaye ni ‘kibaraka’ wa gavana,’ alisema Bw Murungi.
“Ikiwa bunge la kaunti lina tofauti zozote na gavana, lazima utambue kuwa pesa hizo hazitatolewa kamwe. Bunge la kaunti linakosa rasilimali,” aliongeza.
Naibu spika huyo wa Seneti alibainisha kuwa mabunge mengi ya kaunti hayana uwezo wa kufanya kazi yao ya kumulika serikali za kaunti kwa sababu yako chini ya Wakuu wa Kaunti.
“Seneti na Bunge la Kitaifa haziwezi kufanya kazi ikiwa tunategemea serikali kuu kutupa pesa kutekeleza jukumu letu au kuendesha usimamizi wa Seneti. Tunataka kushughulikia mabunge 47 ya kaunti jinsi Serikali ya kitaifa inavyoshughulikia Mabunge yote mawili,” akasema.
Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot alisema mswada huo unanuia kutoa njia ambayo pesa zinazotengewa mabunge ya kaunti zitatolewa huku nia ikiwa ni kuhakikisha kuwa mabunge ya kaunti yana uwezo wa kupata pesa hizo hitaji linapotokea bila kutegemea hazina za kaunti pekee.
“Ni makosa sana kwetu kuketi hapa kama Maseneta kwa miaka 12 iliyopita na kuruhusu wenzetu katika mabunge ya kaunti kwenda na bakuli la kuomba kwenye akaunti za hazina ya kaunti. Inahujumu kikamilifu uhuru wao na majukumu yao,” akasema kiongozi huyo wa walio wengi katika Seneti.
‘Ni vigumu sana kupiga darubini mtu yeyote anayekulisha au mtu yeyote ambaye ana ufunguo wa rasilimali zako. Ninaamini kuwa Mswada huu utawezesha kaunti kupata kumulika kwa kina wakiwa na uhuru wa kusimamia masuala ya kifedha utakapoidhinishwa kuwa sheria,” aliongeza Seneta wa Migori Eddy Oketch.
Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alisema kuwa mabunge ya kaunti kwa sasa yamebanwa katika majukumu yao ya kuchunguza serikali za kaunti kwa sababu magavana wanawahujumu kwa kuwanyima pesa.
“Nimeona visa ambapo gavana anataka kudhibiti uongozi wa Bunge. Kwamba usipokubaliana na matakwa ya mkuu wa kaunti, naye anaweza kuamua kuwa Bunge litasimama. Shughuli zote zitasimama,” akasema Bw Sifuna.
Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA