Habari Mseto

Matiba alirudisha shamba alilonyakua kujenga shule, mahakama yaambiwa

April 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MENEJA mkuu wa kampuni ya Muchanga Investment Limited (MIL) Bw Dimitri Da Gama Rose aliambia mahakama kuu Alhamisi kwamba mwanaharakati wa uzinduzi wa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa na waziri wa zamani marehemu Kenneth Njindo Matiba alirudisha ardhi aliyokuwa amenyakua kujenga Shule ya Hillcrest Group of Schools katika la shamba la ekari 134 lililoko mtaani Karen eneo la Karen.

Dimitri alimweleza Jaji Elijah Obaga kwamba baada ya Bw Matiba kugundua kwamba sehemu ya shamba alilokuwa amejumuisha katika shamba alikojenga shule za Hillcrest Group of Schools ni ya MIL alilirudisha.

“Maafisa wa usoroveya walirekebisha mpaka na kurudisha sehemu ya ardhi iliyokuwa imetwaliwa na kujumuishwa katika ardhi ya shule za Bw Matiba,” alisema Dimitri.

Meneja huyo aliyemweleza Jaji Obaga aliachiwa rekodi zote za shamba hilo na marehemu baba yake Horatius Da Gama Rose alisema awali msimamizi wa shule hizo za Hillcrest Bi Susan Mwamto, bintiye Matiba aliita afisa wa usoroveya kurekebisha mpaka kati ya shule hiyo na shamba hilo la MIL.

Lakini MIL kupitia kwa wakili Mwaniki Gachoka ilihoji kuhusu ardhi iliyokuwa imekatwa na kuunganishwa na shamba la Bw Matiba aliyekuwa ameuziwa na Bw William Berliam Worner na ambaye alikuwa ameinunua kutoka kwa Bw Grattham Biddulph Norman.

Bw Norman alimwuzia Bw Worner ekari 20.2 ambazo ziliuziwa Bw Matiba baadaye ndipo ajenge shule za Hillcrest.

Dimitri alitoa stabadhi mbali mbali kuthibitisha kwamba Bw Matiba alikuwa amethibitisha shamba hilo linamilikiwa na MIL.

Pia alisema Wizara ya Ardhi , Kampuni ya Kenya Power & Lighting, Mamlaka ya Ushuru (KRA), Kaunti ya Nairobi na Makampuni mbali mbali zilitambua kwamba shamba hilo ni la MIL.

“Kile unaeleza hii mahakama ni kwamba Bw Matiba, Wizara ya Ardhi na Idara za Serikali zilitambua MIL kuwa mmiliki wa shamba hili la ekari 134 liloko eneo la Karen,” wakili Cecil Miller alimwuliza Dimitri.

“Ndio na hata natoa riziti za malipo ya ada kati ya 1978 hadi 2013 kuthibitisha Serikali iliipa MIL hati ya umiliki wa shamba hili kwa njia halali,” alijibu Dimitri.

Dimitri , mwanawe marehe Horatius Da Gama Rose aliyemiliki MIL akiwa na aliyekuwa makamu wa Rais Moody Awori aliomba mahakama iamuru kampuni na watu binafsi wanaodai umiliki wa shamba hilo hawana haki ya kuidai.

Kesi inaendelea.