• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
Mchina ndani kwa kuuza vifaa feki vya corona

Mchina ndani kwa kuuza vifaa feki vya corona

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI Mkuu wa kampuni moja ya Uchina alishtakiwa Jumatatu kwa kuuza bidhaa feki za kupima ugonjwa wa corona.

Zhuo Wu almaarufu Williams ni mmiliki wa kampuni ya Zankem Medical Supplies Limited iliyo na afisi zake mtaani Kileleshwa, Nairobi.

Raia huyo wa China alikuwa miongoni mwa washtakiwa waliofikishwa katika mahakama ya Milimani, Nairobi siku ya kwanza ya kufunguliwa tena kwa shughuli za kusikizwa kwa kesi.

Alikabiliwa na mashtaka mawili mbele ya Hakimu Mwandamizi, Bi Zainab Abdul. Alikanusha mashtaka na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

Kiongozi wa mashtaka hakupinga ombi la Wu ila aliomba pasipoti yake isalie na afisa anayechunguza kesi hiyo. Hakimu alimwachilia kwa dhamana ya Sh500,000.

Mshtakiwa alikana kupatikana na vifaa feki vya kupima ugonjwa wa corona mnamo Juni 12, 2020. Kesi itasikizwa Juni 26, 2020. Shughuli za kusikizwa kwa kesi katika Mahakama ya Milimani zilirejelewa jana baada ya kusitishwa kwa miezi mitatu. Utaratibu mkali wa kuwakagua mawakili, washukiwa na kila mtu anayeingia katika jengo hilo uliwekwa huku mahema sita yakiwekwa kuwashughulikia wote waliotaka kuingia.

Washtakiwa na mawakili walisimama katika milolongo mirefu kukaguliwa kwanza kabla ya kuruhusiwa kuingia katika eneo la maegesho ya magari ama ndani ya jengo la mahakama hiyo yenye shughuli nyingi.

Huku haya yakijiri, Kiongozi wa Wengi katika bunge le Seneti, Bw Samuel Poghisio alimtembelea Jaji Mkuu David Maraga katika Mahakama ya Juu.

Mkutano huo wa faragha ulifanywa wiki moja baada ya hotuba kali aliyotoa kinara huyo wa mahakama akieleza mahangaiko aliyopata akitafuta nafasi ya kuzugumza na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu uteuzi wa majaji 41.

Hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani, Bw Francis Andayi aliwahutubia mawakili, washukiwa na wananchi waliofika kortini jana na kuwaeleza kuhusu kanuni mpya. “Lazima mwongozo uliotangazwa na Wizara ya Afya na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ufuatwe na kila mmoja,” akasema.

Bw Andayi aliwaeleza waliofika kortini jana kuwa lazima kila mmoja apimwe joto na kuosha mikono.

You can share this post!

‘Raila alipanga kutenga Pwani na Kenya’

Korti yakataa ombi kufukua aliyekufa kwa corona

adminleo