Mchujo mpya kwa wavuvi 4000 kabla ya kufidiwa na LAPSSET
NA KALUME KAZUNGU
WAVUVI zaidi ya 4000 walioathiriwa na ujenzi wa mradi wa bandari mpya ya Lamu (LAPSSET) sasa watalazimika kupitia upya mchujo kabla ya kuidhinishwa kupokea fidia kutoka kwa serikali.
Akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kukamilisha shughuli ya kukusanya deta kuhusiana na wavuvi walioathiriwa na mradi wa LAPSSET eneo la Lamu Jumatatu, Afisa Msimamizi wa Masuala ya Uvuvi Kaunti ya Lamu, Simon Komu, alisema shughuli ya ukaguzi na kuidhinishwa upya kwa wavuvi husika inalenga kuwatambua wavuvi halisi na pia kufutilia mbali wavuvi feki ambao wamekuwa mstari wa mbele kudai fidia kutoka kwa serikali.
Bw Komu alisema shughuli hiyo itafanywa kwa njia ya wazi, haki na uwajibikaji na kwamba orodha itakayoafikiwa ni ile ya waathiriwa halisi wa mradi huo.
Alisema shughuli hiyo itahusisha kikamilifu jamii ya Lamu hasa wavuvi wenyewe pamoja na viongozi wao na kwamba anaamini orodha itakayoafikiwa itakuwa halali.
Alisema mara nyingi kumeshuhudiwa mtindo wa watu ambao hawajaathiriwa kwa njia yoyote na miradi ya kitaifa hapa nchini lakini kwa njia moja au nyingine wameweza kupenya na kupokea mgao wa fidia wasiostahili.
Alisema ukaguzi na uidhinishaji upya wa wavuvi unaolengwa utazuia visa kama hivyo.
“Tayari tumekamilisha zoezi lililokuwa likiendelea la ukusanyaji wa deta ya wavuvi wote wa Lamu ambao wanadai kuathiriwa na LAPSSET. Tumepokea idadi kubwa ya wavuvi waliojitokeza kujaza fomu husika.
Hata hivyo lazima watambue kuwa hatua hiyo si mwisho. Wavuvi wote watastahili kupitia mchujo.Watakaguliwa na kuidhinishwa kabla ya kupasishwa kupokea fidia. Hii inamaanisha wavuvi ambao si halali watatemwa ilhali wale ambao ni halali wakipasishwa,” akasema Bw Komu.
Mnamo Mei 1 mwaka huu, Mahakama Kuu ya Malindi iliamuru serikali kuwalipa wavuvi 4,734 ambao wanaaminika kuathiriwa na mradi wa LAPSSET kima cha Sh 1.76 bilioni.
Bw Komu aidha alisema idadi hiyo huenda ikaongezeka au kupungua punde shughuli ya ukaguzi na uidhinishaji wa wavuvi halisi itakapokamilika katika kipindi cha juma moja lijalo.