Meneja atetea kampuni kuhusu umiliki wa shamba la Sh8 bilioni
Na RICHARD MUNGUTI
MENEJA mkuu wa kampuni inayomilikiwa na aliyekuwa makamu wa rais Moody Awori Jumatatu alitetea hatimiliki iliyopewa na Wizara ya Ardhi.
Bw Dimitri Da Gama Rose, mwanawe , Horatius Da Gama Rose mmiliki mwenza wa kampuni ya Muchanga Investments alimweleza Jaji Elijah Obaga kwamba shamba hilo lililoko mtaa wa Karen la ekari 135 linamilikiwa kwa njia halali na kampuni hiyo.
“Hati ya umiliki wa shamba hili ilitolewa kwa Muchanga na Wizara ya Ardhi mnamo 1983 baada ya Benki ya Barclays kuiuzia kulingana na wosia aliokuwa ameacha Bw Arnold Braddley aliyeuziwa shamba hilo miaka 90 iliyopita,” alisema Dimitri.
Dimitri aliyekuwa akitoa ushahidi kuhusu umiliki wa shamba hilo lililo na hati miliki tatu alisema mmiliki wa kwanza wa shamba hilo alikuwa Bw Gratthan Biddulph Norman ambaye mwaka wa 1922 alikuwa amepewa ardhi hiyo ya ekari 160.
Baada ya kuziwa shamba hilo 1928 , mlowezi Braddley alikata ekari 20.2 na kumuuzia Bw William Berliam Worner na kusalia na ekari 139.2.
Hatimaye Braddley alimkabidhi bintiye Bi Arnette Theresa Benson ekari nne na kusalia na ekari 134 alizozikabidhi benki ya Barclays kuzisimamia kwa vile alikuwa amezeeka.
Jaji Obaga alifahamishwa kwamba Mabw Awori na marehemu Da Gama Rose walipokea mkopo kutoka kwa Benki ya Barclays kisha wakamaliza kulipa mnamo 1983 ndipo shamba hilo likasajiliwa kwa jina la kampuni ya Muchanga Investments Limited (MIL).
Dimitri aliyekuwa anatoa ushahidi katika kesi ambapo MIL imeshtaki kampuni ya Telesource Com Limited inayomilikiwa na aliyekuwa meneja mkuu wa Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) Josephat Konzollo aliambia korti rekodi iliyoko katika wizara ya ardhi inadhihirisha kwamba shamba hilo ni la Muchanga na wala sio ya walalamishi wengine.