Msipoonyesha uaminifu kwa Ruto na Raila kitawaramba, Aladwa aambia wabunge wa ODM
MBUNGE wa Makadara George Aladwa amewaonya viongozi waliochaguliwa kupitia ODM wakome kuzua maswali kuhusu serikali jumuishi kati ya Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga.
Bw Aladwa ambaye ni mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Nairobi amesema kuwa upinzani na chama tawala, zinafanya kazi pamoja na hakuna kiongozi ambaye anastahili kuwakemea Raila na Rais Ruto kwa kukubali kufanya kazi pamoja.
Bw Aladwa akiongea katika Kanisa la African Divine, Nairobi, Jumapili alisema viongozi ambao wanapinga serikali hiyo wapo katika hatari ya kupoteza umaarufu wao kisiasa.
Ibada hiyo pia ilihudhuriwa na Rais Ruto, Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.
“Kuna baadhi ya viongozi ambao wanapinga serikali jumuishi ya Rais Ruto na Bw Odinga. Nataka nikuhakikishie kuwa tutafuata mwelekeo wako mnamo 2027,” akasema Bw Aladwa .
Mbunge huyo alisema kuwa kutimuliwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ni onyo kwa viongozi ambao wanaeneza ukabila. Alimlaumu Bw Gachagua kwa kumvuga Bw Sakaja ambaye alikuwa na ndoto ya kubadilisha Nairobi.
“Gavana Sakaja hakutuma ombi azaliwe Mluhya na kwa sasa atasalia kuwa Gavana wa Nairobi. Nimehudumu kama Meya hapa hapo awali na kama Mluhya sina nia ya kutoa matamshi yanayowagawanya nchi,” akaongeza
Bw Aladwa anahudumu muhula wa pili katika Bunge la Kitaifa na alimtaka Rais William Ruto asipoteze dira kutokana na watu ambao wanampinga akiwahudumia Wakenya.
“Tutakuunga mkono Rais na wale ambao wanaeneza umbeya waendelee kufanya hivyo lakini sisi tupo nyuma yako kama ODM,” akasema.
Wakati wa ibada hiyo, viongozi wa ODM walitoa wito kwa Rais aendelee kumpigia debe Bw Odinga ambaye ana nia ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika mwakani (AUC).
Aidha Bw Aladwa alitoa wito kwa Rais ahakikishe kuwa anafanya kazi na viongozi wote wa eneo la Magharibi ili kuhakikisha ustawi na maendeleo ya eneo hilo.
“Mtoto wetu Mudavadi amefanya kazi na wewe siku zote. Hakikisha mahali utamweka katika uchaguzi mkuu wa 2027 na tutakuwa na wewe,”akasema.
Bw Aladwa miezi miwili iliyopita aliwaongoza viongozi wa ODM Kaunti ya Nairobi kuzuru ikulu ambapo walijadiliana na Rais kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo na ushirikiano wa kisiasa.