Mudavadi adai Raila aliwaficha kuhusu muafaka
Na VALENTINE OBARA
KIONGOZI wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, ameibua shaka kuhusu kama Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga alikuwa mwaminifu kwa vinara wenzake wa NASA kabla aungane na serikali.
Kulingana na Bw Mudavadi, uamuzi wa Bw Odinga kushirikiana na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta uliashiria kuwa wawili hao walikuwa wakishauriana kwa muda mrefu bila vinara wengine wa NASA kujua.
“Hakuna jinsi angechukua hatua aina hii ghafla. Ni wazi mipango hiyo ilikuwa ikiendelezwa kwa muda mrefu ilhali mimi kibinafsi sikufahamu,” akasema kwenye mahojiano Jumapili usiku katika Runinga ya NTV.
Kwenye mahojiano tofauti, Bw Odinga amewahi kuthibitisha kuwa hatua yake kushirikiana na Rais Kenyatta ilikuwa siri yao wawili ingawa haifahamiki walikuwa wakishauriana kwa muda gani.
Waziri huyo mkuu wa zamani pia amekuwa akikosolewa na wenzake wanaodai alienda kula kiapo kuwa ‘rais wa wananchi’ katika uwanja wa Uhuru Park walipokuwa wakimsubiri kwingine.
Bw Mudavadi alimwonya Bw Odinga na Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuhusu ushirikiano wao na serikali akasema hatafuata mkondo huo bali chama chake kitatekeleza majukumu ya upande wa upinzani nchini.
Kulingana na makamu huyo wa rais wa zamani, hakuna ubaya kwa viongozi wa pande tofauti za kisiasa kushirikiana lakini kuna hatari kubwa wakati ushirikiano huo unapotishia kuangamiza upinzani.
“Hatufai kuonekana kwamba sote sasa tunafululiza kujiunga na serikali. Jubilee inakumbwa na matatizo mengi serikalini na hatustahili kuwa washirika wake katika makosa inayofanya,” akasema.
Wiki iliyopita, Bw Musyoka alitangaza kuwa wanachama wa Wiper walikubaliana kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta, na wabunge wake wakaagizwa kuunga mkono ajenda za serikali wakiwa bungeni.
Hata hivyo, Bw Mudavadi alisema uamuzi wake haumaanishi amekosana na Bw Odinga kwani wote wana haki ya kuchukua misimamo tofauti kisiasa.
Alisema muafaka ulikuwa muhimu kutuliza taharuki nchini lakini haamini una uwezo wake kuleta mabadiliko ikizingatiwa kuwa Bw Odinga aliwahi kuchukua hatua sawa na hiyo wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 alipoungana na aliyekuwa rais Mwai Kibaki.
“Muafaka wa 2007/2008 ulitokana na wizi wa kura. Wakati huu pia ulitokana na uchaguzi tatanishi. Ni wazi katika ile miaka mitano changamoto iliyokuwepo haikutatuliwa. Sasa mwaka mmoja umekamilika na hatuoni kama kuna juhudi za kusuluhisha mizozo ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka,” akaeleza.
Kuhusu uchaguzi ujao wa 2022, Bw Mudavadi alisema si lazima aungwe mkono na Bw Odinga wala kinara mwingine yeyote wa NASA ili ashinde urais bali atajitahidi kushawishi wananchi kuhusu uwezo wake wa kuongoza taifa.
Kumekuwa na fununu kwamba vinara wa muungano huo walikubaliana kumuunga mkono Bw Odinga kwa msingi kuwa atamuunga mkono mmoja wao 2022, ingawa ODM husisitiza kitakuwa na mgombeaji wake wa urais.