Mwanahabari ashambuliwa akifuatilia habari za kutimuliwa kwa Gachagua
MWANAHABARI anayehudumu Kaunti ya Nyeri amelazwa hospitalini baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana alipokuwa akifuatili hisia za wakazi baada ya Naibu RaisRigathi Gachagua kutimuliwa na Bunge la Kitaifa.
Sam Kiere, mwanahabari wa kituo cha TV47 alijeruhiwa akifanya kazi pamoja na ripota William Moige mjini Karatina, ngome ya Bw Gachagua, Jumanne jioni.
Walishambuliwa na wanaume wanaoaminika kuwa maafisa wa polisi ambao hawakuwa wamevalia sare rasmi, waliowasili kwa gari aina ya Subaru.
Licha ya kilio cha wanahabari hao, polisi waliovalia sare waliokuwa wakipiga doria mitaani Karatina hawakuingilia kati.
Washambulizi hao pia walichukua kamera na vifaa vingine vya kituo hicho cha runinga.
“Walitulazimisha kukatiza upeperushaji wa moja kwa moja tulipokuwa tukikusanya maoni kutoka kwa wakazi.”
“Walikuwa na Subaru isiyokuwa na nambari ya usajili sawa na magari yanayotumiwa na Idara ya Uchunguzi kuhusu Uhalifu (DCI),” alisema Bw Moige.