Mzee Wanjigi hafai kuamriwa afike kortini – Mawakili
Na RICHARD MUNGUTI
ALIYEKUWA Waziri Bw Maina Wanjigi hatafika kortini hivi karibuni kujibu mashtaka ya kutopata cheti cha umiliki wa silaha.
Jaji Roselyn Aburili aliamuru mahakama ya Nyeri isiendelee na kesi dhidi ya mwanasiasa huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 87 aliyekuwa mbunge wa Kamkunji kwa miongo kadha.
Jaji Aburili alifahamishwa kuwa polisi wamekuwa wakisumbua familia ya Bw Wanjigi na kwamba haki zao zimekiukwa.
Mawakili Kiogora Mugambi , Nelson Havi na John Khaminwa walimweleza Jaji Aburili kwamba Mzee Maina yuko Uingereza akipokea matibabu na kwamba amri afike katika mahakama ya Nyeri kujibu mashtaka hayafai.
Jaji Aburili alikubaliana na mawakili Khaminwa, Havi ,Orengo na Kiongora kwamba wamethibitisha haki za Maina zimekiukwa.
Jaji huyo aliamuru mawakili hao wawasilishe kesi kamili katika muda wa siku 14 ndipo wawasilishe ushahidi kwamba serikali inawasumbua Mzee Maina Wanjigi.
Khaminwa alisema, “Hakuna ukiukaji mwingine wa hali ya juu wa haki za Mzee Maina Wanjigi kama kumweleza afike kortini akiwa mngonjwa.”
Alisema polisi walivamia makazi ya mwanawe mtaani Muthaiga Oktoba 17, 2017 wakidai wanasaka silaha.
Jaji mwingine wa Mahakama kuu George Odunga pia amezima hatua ya kumshtaki Bw Jimi Wanjigi.