• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Onyo kwa wanaouza dawa za hospitali za umma

Onyo kwa wanaouza dawa za hospitali za umma

Na BRIAN OCHARO

SERIKALI ya Kaunti ya Taita Taveta imenunua dawa za thamani ya zaidi ya Sh39.5 milioni kuboresha huduma za afya.

Akiongea katika hafla ya kugawa hizo dawa, Waziri wa Afya katika kaunti hiyo  Dkt Frank Mwangemi ametoa onyo kwa wauguzi wa afya kuwa watachukuliwa hatua ya kisheria wakipatikana wakiziuza.

Alisema serikali ya kaunti inapeleleza madai ya ulaghai kuhusu uuzaji dawa.

“Gavana ameongea na EACC kusaidia kujua jinsi dawa zimekuwa zikipotea kwenye vituo vyetu vya afya. Wahusika wakijulikana watakabiliwa kisheria,” alisema Bw Mwangemi.

Waziri huyo alisema wauguzi wa afya ambao huenda wakapatikana na kosa la kuuza dawa za umma watafutwa kazi na hatua pia washtakiwe.

Wakiongozwa na Kiongozi wa wengi katika bunge la Kaunti, Bw Jason Tuja, viongozi wa kaunti waliapa kudhibiti visa hivyo, ambavyo kwa muda vimekuwa vikishuhudiwa.

Bw Tuja amesema ni sharti kwa huduma zinazotolewa kwa hospitali ya rufaa ya Moi mjini Voi kufikia kiwango cha kitaifa na kuongeza kwamba wako tayari kama bunge la kaunti kuidhinisha bajeti itakayopendekezwa na waziri wa afya.

“Kama uko hapa na unahusika na madawa kupotea, ole wako kwasababu tunakumulika. Sharti madawa yahudumie mwananchi. Kwa wewe uliye na duka la kuuza madawa na unadhania utatumia hospitali hii kujifaidi, unajidanganya na ufunganye virago uondoke mapema,” alisema Bw Tuja.

Usemi wake umewekwa uzani na mwakilishi wodi wa Mwatate, Bw Abednego Mwanjalla ambaye alitaka visa vya wagonjwa kurejeshwa manyumbani kwa kukosekana wauguzi kushughulikiwa kwa haraka ili visa vya wagonjwa kusaka huduma kwa taasisi binafsi kupungua.

Afisa mshirikishi wa shirika la usambazaji madawa KEMSA Dagane Dabra, alipongeza ushirikiano wa karibu kati ya shirika lake na serikali ya kaunti hiyo na kusema wako imara kuhakikisha kaunti haitashuhudia upungufu wa madawa.

 

You can share this post!

Tetesi kasisi alitumia ndumba kupora mke

Malori yenye magunia 330 ya makaa yanaswa

adminleo