Habari Mseto

Ruto: Wanaume, kina mama wanaonyonyesha wapeni muda wapumue, tulizeni boli

Na SAMMY WAWERU March 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto amewataka wanaume hususan wanaoishi mitaa ya mabanda kuwapa muda wake wao wanaonyonyesha badala kukimbilia kuongeza idadi ya watoto.

Akihutubia umma katika mtaa wa Kibra, jijini Nairobi, mnamo Alhamisi, Machi 13, 2025, kiongozi wa nchi alielezea haja ya kina mama kupewa muda kulea watoto wachanga.

Kibra ni mojawapo ya mitaa mikubwa ya mabanda nchini.

Wakenya wakiendelea kulalamikia kuhusu gharama ya juu ya uchumi na maisha, Dkt Ruto alisema anasikitishwa na wanaume ambao hawawapi muda bibi zao – haswa wanaonyonyesha, wakiwataka kuongezea watoto.

Akitumia lugha iliyosheheni ucheshi, Rais pia aliwataka wanawake kuwa na subira na kukumbatia mbinu za uzazi.

“Kama ananyonyesha, tulia kidogo… Unakimbia mbio, unaenda wapi?” Rais Ruto alihoji.

Maelezo yake yakisababisha umma kuangua kicheko, Rais alidai “amepokea malalamishi ya wanawake kuwa bwana zao wanawapeleka mbio katika masuala ya uzazi.”

“Hawa wanaume, kina mama wanalalamika mnawasumbua,” Ruto alisema, umma ukiangua kicheko.

Matamshi hayo yanaashiria kuwa wanaume wanawapeleka kwa mwendo wa kasi wanawake kwenye masuala ya mahaba, na endapo hawajakumbatia mbinu za kudhibiti uzazi wanaishia kushika mimba.

Mitaa ya mabanda kwa sababu ya gharama yake nafuu ya nyumba, wananchi wenye mapato ya chini hukita kambi humo kujiendeleza kimaisha.

Isitoshe, wakazi wa mitaa ya mabanda wanahusishwa na dhana ya kuishi bila upangaji uzazi kwa sababu ya umaskini hivyo basi kuwa na idadi ya juu ya watoto.