SAKATA YA NYS: Washukiwa 24 kusalia ndani kwa siku 7
Na BENSON MATHEKA
WASHUKIWA 24 wa sakata ya wizi wa mabilioni kutoka Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS) watakaa seli kwa takriban wiki moja wakingoja uamuzi wa ombi lao la kutaka wapewe dhamana na mahakama.
Kuna uwezekano kuwa washukiwa hao wanaweza kufunguliwa mashtaka zaidi.
Jumatano, Katibu wa kudumu wa Wizara ya Utumishi wa umma, Vijana na Michezo Lilian Mbogo Omollo, mmoja wa walioshtakiwa Jumanne, alilazwa katika Hospitali Kuu ya Kenyatta baada ya kuugua akiwa rumande.
Bi Mbogo aliugua akiwa gereza la wanawake la Lang’ata saa chache baada ya mahakama kukataa kuachilia washukiwa wa kashfa hiyo kwa dhamana.
Saa chache baada ya kulazwa, Mawakili wake walifika kortini wakitaka agizo ahamishiwe hospitali chaguo lake.
Upande wa mashtaka ulisema kwamba washukiwa wote wanaendelea kuchunguzwa na idara tofauti za serikali na ndani ya NYS kwa kushukiwa kuhusika na visa vingine tofauti vya ulaghai.
Kwenye hati ya kiapo ya kupinga kuachiliwa kwa dhamana kwa washukiwa hao akiwemo Katibu wa kudumu wa wizara ya vijana na michezo Lilian Mbogo Omollo na Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai, polisi walisema huenda wakaingilia uchunguzi huo.
Mahakama iliambiwa kwamba uchunguzi unahusu nyanja mbali mbali za maisha na kwa hivyo washukiwa ni hatari kwa usalama wa taifa.
“Uchunguzi unahusu nyanja mbali mbali za maisha na ni wazi kuwa washukiwa ni hatari kwa usalama wa taifa, maslahi ya nchi na raia kwa jumula,” ilisema hati ya kiapo ambayo upande wa mashtaka uliwasilisha kortini kupinga dhamana kwa washukiwa.
Wapelelezi wanahisi kwamba vitendo vya washukiwa na washirika wao vinahatarisha usalama na amani na wanafaa kuzuiliwa rumande hadi kesi itapoamuliwa.
Kutokana na vyeo vya washukiwa na hadhi yao katika jamii, upande wa mashtaka unasema ni rahisi kuingilia mashahidi katika kesi hiyo wakiachiliwa kwa dhamana.
Kutisha mashahidi
“Washukiwa wote ni watu walio na ushawishi na wanashikilia nyadhifa za juu katika jamii, hivyo basi wanaweza kuwatisha mashahidi,” upande wa mashtaka ulieleza mahakama kwenye hati ya kiapo.
Kulingana na hati hiyo, mashahidi wanatoka wizara ya utumishi wa umma, vijana na michezo ambayo washukiwa wanashikilia nyadhifa za juu na kuachiliwa kwao kwa dhamana kunaweza kuvuruga kesi.
Kwenye hati hiyo, kiongozi wa uchunguzi, Mike Muia kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), anasema kwamba uchunguzi kuhusu sakata hiyo ulifuatia ripoti za ujasusi.
Bw Muia anaeleza kwamba uchunguzi ulianza Aprili 26 baada ya DCI kupokea ripoti za ujasusi kuhusu vitendo vya ulaghai katika NYS.
Mbali na Bi Mbogo na Bw Ndubai, wafanyakazi wengine wa NYS walioshtakiwa wanatoka idara za uhasibu, fedha, ununuzi, usimamizi na ukaguzi.
Wengine walioshtakiwa ni wafanyabiashara ambao walidaiwa kupokea mamilioni ya pesa kutoka idara hiyo bila kuuza bidhaa zozote. Miongoni mwao ni Lucy Wambui Ngirita aliyedaiwa kupokea Sh56 milioni na Ann Wambere Ngirita aliyedaiwa kupokea Sh59 milioni bila kuuza chochote.
Washukiwa wanazuiliwa rumande hadi Juni 5 mahakama itakapoamua iwapo wataachiliwa kwa dhamana.