Habari Mseto

Serikali yaamriwa kuwalipa wavuvi mabilioni

May 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu imeamuru serikali iwalipe fidia ya Sh1.76 bilioni wavuvi wapatao 4,600 katika kaunti ya Lamu.

Wavuvi hao watafaidika kutokana na mradi wa ustawishaji wa Bandari ya Lamu na ujenzi wa barabara zitakazohudumia mataifa ya Sudan na Ethiopia (LAPSET).

Majaji Pauline Nyamweya, Joel Ngugi , Beatrice Jaden na John Mativo walisema Wavuvi hao wanafaa kulipwa fidia kwa sababu eneo walilokuwa  wanatumia kuvua samaki lilivurugwa.

Majaji hao waliiamuru Serikali iwalipe Wavuvi hao fidia hiyo katika muda wa mwaka mmoja kuanzia Aprili 30, 2018.

Majaji Nyamweya , Ngugi , Jaden na Mativo walisema Wavuvi hao hawafaidi tena kwa vile eneo walilotegemea kuvua samaki na kuuza kujipatia riziki sasa ndipo mradi wa LAPSET unaendelea.

“Kuchelewesha kuwalipa fidia Wavuvi fidia hii itakuwa ni ukiukaji wa haki zao na ubaguzi sawia na kuwanyima riziki yao,” walisema majaji hao wanne.

Mahakama iliamuru fidia hiyo ilipwe wakati mmoja na ufadhili wa mradi huo kama ilivyoidhinishwa katika ulipwaji fidia wa Uvuvi katika mradi huo.

Ikitoa uamuzi wa kesi iliyowasilishwa na Mvuvi Mohammed Ali Baadi ikipinga ustawishaji wa mradi huo wa LAPSET utakaogharimu Sh2.6bilioni , Mahakama ilisema maoni ya wavuvi hayakuzingatiwa kabla ya kazi kuanza katika bandari hiyo ya Lamu ambapo walikuwa wakivua Samaki wanaouza kujikimu kimaisha.

Mahakama ilisema Serikali haikuwafidia ardhi yao licha ya madhara iliyosababisha katika mazingira.

Karika kesi hiyo iliyowasilishwa mahakamani mnamo 2012 Wavuvi hao walisema uchimbaji katika bahari ya Hindi uliathiri misitu, nyasi, ufuo wa bahari ambako Kobe na Samaki huzalia.

Serikali imeagizwa itayarishe ramani ya kuhifadhi ya Kisiwa cha Lamu kilicho Makavazi ya kimataifa kama kinavyotambuliwa na shirika la UNESCO katika kipindi cha muda wa mwaka mmoja.