Habari Mseto

Sheria mpya ya majani chai iidhinishwe haraka – Wakulima

December 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WAKULIMA wa majani chai wamepata zawadi ya Krismasi baada ya maseneta kupitisha mswada utakaoleta mageuzi yatakayowaongezea mapato na kukinga dhidi ya unyanyasaji na matapeli walioteka sekta hiyo.

Wakulima hao sasa wanataka Rais Uhuru Kenyatta kutia saini sheria hiyo mpya wakisema itawakomboa kutoka mawakala ambao wamekuwa wakifurahia jasho lao kwa miaka mingi.

Katika kikao maalum cha Jumatatu maseneta wote 33 waliohudhuria, walipiga kura ya kuunga mkono Mswada wa Chai jinsi ulivyofanyiwa marekebisho na bunge la kitaifa.

Maseneta hao waliunga mkono ripoti ya kamati ya seneti kuhusu kilimo iliyopendekeza waupitishe ili wakulima waanze kuvuna manufaa yake haraka iwezekanavyo.

“Ingawa bunge la kitaifa limefanya marekebisho 30 katika mswada huu, mageuzi makubwa yenye manufaa kwa wakulima yamedumishwa. Kwa hivyo, kamati yangu inawaomba tuupitishe bila kupendekeza marekebisho mengine ili wakulima wafaidi. Wenzetu na wadau wengine ambao hawakuridhika na sehemu za mswada wasife moyo kwani bado nafasi itapatikana kwao kuifanyia marekebisho sheria hii wakati mwingine,” akasema mwenyekiti wa kamati ya seneti kuhusu kilimo Njeru Ndwiga.

Kauli yake iliungwa mkono na maseneta Kiranja wa wengi Irungu Kang’ata, kiongozi wa wachache James Orengo, Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Moses Wetang’ula (Bungoma), Johnson Sakaja (Nairobi), miongoni mwa wengine.

Seneta wa Kericho, Aaron Cheruiyot ambaye ni mdhamini wa mswada huo aliwapongeza maseneta wenzake kwa kuupitisha.’Ama wa kweli siku kuu ya Krismasi imejiri mapema kwa wakulima wetu wa majani chai.

“Kwa kupitisha mswada huu tumewakomboa kutoka kwa minyororo ya Shirika la Ustawishaji wa Chai Nchini (KTDA) na matapeli wengi ambao hula jasho lao. Sasa watapata faida kutokana na jasho lao,’ akasema.

Mswada huo ambao sasa unasubiriwa kutiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta, unalenga kunyoosha sekta ya majani chai na kurejesha usimamizi wake chini ya Bodi ya Chai Nchini (TBK).

Sheria hiyo kimsingi, inapokonya KTDA usemi katika usimamizi wa sekta hiyo, hasa uuzaji wa zao hilo katika mnada wa Mombasa na masoko ya ng’ambo.Isitoshe, sheria hiyo itaweka usimamizi wa viwanda vidogo vya majani chai, mnada wa chai wa Mombasa na asasi zote katika sekta ya bodi hiyo.

TBK itakayosimamiwa na serikali kuu, ndio itatunga kanuni za kusimamia asasi zote za sekta ya chai nchini. Sekta hiyo iliondolewa chini ya usimamizi wa serikali kuu mnamo mwaka wa 2000.

Kanuni mpya za uzalishaji na uuzaji wa majani chai pia zitaanza kutekelezwa, chini ya sheria hii kando na kuondolewa kwa ada nyingi ambayo KTDA imekuwa ikiwatoza wakulima.

Kwa mfano, Sh3 kwa kila kilo ya majani chai inayouzwa, ambazo hutozwa wakulima katika bonasi yao kila mwaka.Kwa mujibu wa mswada huo, pesa zitakazopatikana kutokana na mauzo ya zao hilo sasa hazitapelekwa kwa akaunti ya KTDA bali katika akaunti ya viwanda vya majani chai.

“Wakulima watapokea asilimia 50 ya mauzo ya zao hilo katika mnada baada ya fedha hizo kupokewa katika akaunti za viwanda huku fedha zilizosalia wakizipokea mwisho wa mwaka,” mswada huo unaeleza.

Vile vile, wakulima watapokea malipo hayo baada ya siku 14 tofauti na hali ilivyo sasa ambapo KTDA huchelewesha malipo hayo kwa hadi mwaka mmoja.

Pesa zilizosaliwa watalipwa mwishoni mwa mwaka wa kifedha.Watakuwa wakipokea malipo hayo, kila mwezi, kutoka kwa viwanda vya majani chai katika maeneo yao.

Chini ya sheria hii TBK ndio imetwikwa wajibu wa kuunda kanuni za utawishaji, usimamizi wa mnada na uuzaji zao hilo ng’ambo.Wakulima wa majani chai walichangamkia mswada huu wakisema utawawezesha kupata faida kutokana na kilimo chao.