Siasa za ugavi wa pesa zachangia kufifia kwa umaarufu wa Ruto Mlima Kenya
NA MWANGI MUIRURI
SIASA za mfumo utakaotumika kugawa Sh316.5bilioni za Kaunti mwaka huu wa kifedha (2020/21) zinatishia umaarufu wa Naibu wa Rais Dkt William Ruto katika Mlima Kenya huku kinara wa ODM Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wakijipa umaarufu eneo hilo.
Wasiwasi kwa kambi ya Dkt Ruto ambaye kwa muda amekuwa akibarehe kwa ufuasi sugu Mlima Kenya ni kwamba hata wandani wake kama mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na mwenzake wa Mathira Rigathi Gachagua wamejitokeza hadharani wakiandamana na wafuasi wa Kieleweke kuhusu mfumo wa ugavi pesa hizo.
Hatari kuu kwa Dkt Ruto Mt Kenya ni kwamba Rais Kenyatta na wandani wake wamekuwa wakisaka mbinu ya kumfunmgia nje ya urithi wa iurais 2022 na sasa ni kama amejitoa kafara kwa njama hizo.
Huku Dkt Ruto akiwa amekataa kuuunga mkono mfumo wa kuzingatia idadi ya watu almaarufu Shilingi moja kwa mtu mmoja unaopigiwa debe na wengi Mlima Kenya, Odinga amejitiokeza akiunga mkono mfumo huo unaoungwa mkono pia na Rais Kenyatta.
Huku Rais akiwa mbioni kujaribu kutwaa ufuasi wa Mlima Kenya kutoka kwa Dkt Ruto, wadadisi sasa wanasema kuwa huenda iwe kazi rahisi ikiwa mfumo huo unaopendekezwa na serikali utaanguka tena katika kura ya Jumanne ijayo ndani ya Seneti.
Katika kura ya Jumanne iliyopita, maseneta 25 walipinga huku 22 wakiunga mkono mfumo huo uliowasilishwa nka kiranja wa wengi, Irungu Kang’ata.
Bw Kang’ata aliambia Taifa Leo kuwa “hali hii inaweza ikaamua ni kina nani wa kupewa ufuasi Mlima Kenya 2022.”
Alisema kuwa Odinga akitusaidia kupitisha hoja hii Jumanne, tutarejesha mkono kwa kupalilia umoja ndani ya Handidsheki yake na Rais na pia tuunge mkono mradi wake wa kisiasa wa BBI na miradi yake ya 2022 bora tu tuwe ndani ya mipango yake.”
Alisema kuwa Dkt Ruto kwa sasa amejitenga na Mlima Kenya katika hali hii ya pesa za Kaunti “na ni vyema aambiwe kuwa ameanza mteremko wa kujihujumu kisiasa kwa kuwa kuna hofu kwamba angetaka kuongoza Mlima Kenya ukiwa na ufukara ndio utii urais wake kwa kutegemea chakula cha misaada.”
Akisema hayo, Bw Gachagua na Nyoro hawakutetea DKt Ruto kama ilivyo kawaida yao, wakiunga mkono usemi wa Kang’ata.
“Marafiki wa kweli hujulikana wakati wa vita. Mlima Kenya uko kwa vita kwa sasa kuhusu haki yetu halisi ya ugavi wa pesa. Wanaotuunga mkono ndio marafiki,” akasema Gachagua huku Nyoro na Kang’ata wakiwa kando wakioneshana kuridhishwa na matamshi hayo.
Hapo jana, Mwenyekiti wa muungano wa Gikuyu, Embu na Ameru (Gema) Kasisi mstaafu Lawi Imathiu alisema kuwa “huu ni wakati wa kudadisi marafiki wetu wa dhati wala sio wale tu wa kujitakia kura zetu.”
Alisema kuwa “marafiki wa dhati kwa jamii zetu ni wale ambao wanatutakia mema katika hali za kupambana na umasikini kupitia ugavi wa hela kufathili maendeleo katika maisha yetu.”
Alisema kuwa “kwa sasa tumeanza kupevuka macho katika mjadala huu wa ugavi wa pesa na tunafuatilia kwa makini sana ni kina nani ambao huwa na mawazo mema kutuhusu na wale ambao haja yao ni kutuchumbia ndio tuwape kura zetu 2022.”
Alisema kuwa wale ambao hawatajitokeza waziwazi kuunga mkono pesa zigawe kwa kuzingatia idadi ya watu basi sio marafiki wa Mlima Kenya kisiasa, kiuchumi na hata kijamii.
Ni wazo ambalo liliungwa mkono na Mwenyekiti wa baraza la wazee Bw Wachira Kiago aliyesema “unafiki wa wanasiasa kuhusu Mlima Kenya sasa ndio unajitoa hadharani.”
Alisema kuwa akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli katika kila hali ya maisha “na kwa sasa tunafuatilia kwa umakinifu mchango wa wawaniaji wa urais 2022 na jinsi wanavyotumia ushawishi wao kusukuma pesa zigaiwe watu wala sio vichaka na wanyama wa pori.”
Wazee hao wawili walisema kuwa Mlima Kenya hautakubali hadaa za kisiasa “na ni lazima utuonyeshe kwa matamshi na vitendo kuwa unaunga mkono kuinuka kwa watu wa Mlima Kenya kiuchumi kabla uanze kutuomba kura zetu.”
Aliyekuwa mkuu wa kiutawala katika maeneo mengi hapa nchini Joseph Kaguthi alisema kuwa “kwa sasa Mlima Kenya unatafuta mtu wa kushirikiana naye ambaye ako na maono ya kupambana na umasikini ambao umekita mizizi eneo hili.”
Aliambia Taifa Leo kuwa “kwa sasa kati ya vinara wakuu wa kisiasa, ni Odinga na Rais Kenyatta ambao wameonekana kujituma kutetea masilahi ya Mlima Kenya huku Dkt Ruto akionekana kuyumba akizingatia kupendwa kwingine nje ya Gema.”
Alisema kuwa hali hiyo ni hatari kwa kuwa bila ufuasi wa maeneo yaliyo na idadi kubwa za watu kama Mlima Kenya, Magharibi na Nairobi “basi sahau urais na hatari kuu kwa hili iko kwa Dkt Ruto mwenyewe ambaye anaonekana sasa kulenga ufuasi wa jamii yake na jamii ndogo zingine hali ambayo ina uhakika wa kumtuma kwa ushindwe wa urais 2022.”