Habari MsetoSiasa

Sina tamaa ya kuendelea kuwa mamlakani baada ya 2022 – Uhuru

October 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta ameondolea wasiwasi viongozi wanaoshuku kuna mipango ya kumwezesha kuendelea kuongoza baada ya 2022.

Rais alipuuzilia mbali mapendekezo ya baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakisema itakuwa vyema kwake kupewa mamlaka mapya kama vile ya waziri mkuu kupitia kwa marekebisho ya katiba ili asalie serikalini baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Pendekezo hilo ni miongoni mwa sababu ambazo zimesababisha mgawanyiko katika chama cha Jubilee ambapo wandani wa Naibu Rais William Ruto, wamekuwa wakimshinikiza rais kutangaza msimamo wake kuhusu urithi wa kiti chake.

Kwenye mahojiano Jumatatu na shirika la habari la CNN, Rais Kenyatta alisema hana nia wala haja ya kutetea marekebisho ya katiba kumwezesha kuendelea kuwa mamlakani baada ya 2022 atakapokamilisha muhula wake wa pili wa uongozi.

“Sina haja kuongoza kwa mara ya tatu. Watu wanajadili kurekebisha katiba si kwa sababu wanataka rais aendelee kuongoza bali kutokana na gharama ya juu ya katiba iliyopo. Hayo ndiyo masuala ambayo yamejitokeza wazi,” akasema.

Ingawa hakufafanua wazi kama ataunga mkono marekebisho ya katiba, matamshi hayo yaliashiria huenda akaunga mkono marekebisho ambayo yatapunguza nyadhifa za kisiasa hasa ikizingatiwa kuwa amewahi kulalamika hadharani kuhusu jinsi mfumo uliopo wa uongozi ulivyo ghali.

Pendekezo la kubuni nyadhifa mpya za waziri mkuu na manaibu wake lilianzishwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga, ambaye anaamini hiyo ni njia ya kutoa nafasi kwa jamii tofauti kuwakilishwa uongozini ili kuzuia taharuki zinazosababisha ghasia za kikabila kila wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Hata hivyo, viongozi kadhaa wa Jubilee hasa wandani wa Bw Ruto, wamekuwa wakipinga pendekezo hilo na kusema ni njama ya kuvuruga mipango ya Bw Ruto kumrithi Rais Kenyatta uchaguzi utakapofanywa.

Rais Kenyatta pia alitetea uamuzi wake wa kushirikiana na Bw Odinga akisema mwafaka wao ulikuwa muhimu kuleta utulivu utakaofanikisha maendeleo.

“Tunahitaji kusonga mbele. Ni kweli kuwa hatutaweza kuelewana kuhusu kila kitu lakini tunaweza kuelewana kuhusu hili suala moja, kwamba siasa zina wakati wake,” akasema.

Mjadala kuhusu hitaji la Rais Kenyatta kuundiwa nafasi serikalini 2022 ulitiwa moto wakati wa sherehe za Leba Dei mwaka huu, pale Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli, alipodai Rais bado ni kijana kwa hivyo inapaswa akabidhiwe wadhifa wa waziri mkuu “atakapostaafu” kutoka kwa urais.

“Tusiporekebisha katiba, kwani mnadhani Uhuru ataenda wapi ilhali yeye bado ni kijana? Lazima tuirekebishe ili tumtafutie nafasi la sivyo atasumbua wale watakaoingia mamlakanni,” alisema Bw Atwoli mnamo Mei 1.