Habari Mseto

Tutapunguza ada ya umeme mradi wa Olkaria ukikamilika – Serikali

June 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na KAZUNGU SAMUEL

KAMPUNI ya kutengeneza umeme nchini, KenGen Jumatatu ilisema kuwa gharama za umeme zinatarajiwa kupungua 2019.

Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Bi Rebecca Miano alisema hii itafanikiwa baada ya kukamilika kwa mradi wa kawi ya mvuke wa Olkaria. Mradi huo unatarajiwa kuongeza megawati 168 za stima, hivyo basi kupunguza gharama za matumizi ya umeme.

“Mradi wa stima ya mvuke katika kituo cha Olkaria sasa umefikia asimilia 40 na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka ujao. Ukikamilika, gharama ya stima inatarajiwa kurudi chini hasa kwa vile utakuwa ukitoa megawati 168,” akasema Bi Miano.

Alisema mradi huo ukikamilika itajulikana ni kwa kiwango gani bei ya stima itapungua.

Naye mwenyekiti wa kampuni hiyo, Bw Joshua Choge alisema kuwa wanalenga kuwa na miradi ambayo itasaidia kuleta kawi nafuu kwa Wakenya wote katika siku za usoni.

“Kampuni kwa sasa imo katika juhudi za kutekeleza stima ya ziada ya megawati 720 kufikia mwaka wa 2020, kulingana na idadi ya mahitaji ya stima ambayo imeongezeka maradufu,” akasema.

Kongamano hilo la siku tano limewaleta wajumbe 500 kutoka kampuni hiyo pamoja na washika dau wengine wa humu nchini na wa kimataifa.

Kongamano hilo liliandaliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2012 lakini sasa limekuwa likifanyika kila siku ambapo sasa wawekezaji wengine katika sekta ya kawi hukutana na KenGen na kutoa mawazo yao kuhusu kuboresha huduma.