Habari Mseto

Viongozi Magharibi wamtaka MaDVD ateuliwe Waziri wa Usalama wa Ndani

Na VICTOR RABALLA November 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI kutoka Magharibi mwa Kenya sasa wanamtaka Rais William Ruto amteue rasmi Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi kama waziri mpya wa usalama wa ndani.

Wamesema kuwa Bw Mudavadi yupo pazuri kurithi wizara hiyo kutoka kwa Profesa Kithure Kindiki ambaye alikwezwa cheo hadi akawa naibu rais.

Seneta wa Kakamega Dkt Bonni Khalwale alisema Bw Mudavadi ameonyesha uongozi bora na sasa anastahili kutwaa uongozi wa wizara hiyo muhimu.

“Tusalie tumeungana nyuma ya Rais ili Mudavadi awe waziri wa usalama wa ndani ndipo aimarishe usalama wa nchi,” akasema Dkt Khalwale.

Alikuwa akiongea katika kanisa la Embukambuli, Khwisero, ibada ambayo pia  ilihudhuriwa na Rais Ruto na Bw Mudavadi.  Kinara huyo wa waziri amekuwa kaimu waziri wa usalama wa ndani na pia anashikilia wizara ya usalama wa ndani.

Kauli yake iliungwa mkono na Mbunge wa Khwisero Christopher Aseka ambaye pia alimpigia upato Bw Mudavadi  akisema anastahili kuepushwa kupaa kutoka taifa moja hadi jingine ndipo amakinikie usalama wa nchi.

Mbunge wa Navakholo Emannuel Wangwe naye alimsifu Bw Mudavadi akisema nyota yake ya kisiasa inayoendelea kungáa itahakikisha kuwa Magharibi inanufaika na utawala wa Kenya Kwanza.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Francis Atwoli alisema kuwa uwepo wa viongozi watatu wakuu kutoka Magharibi mwa Kenya katika utawala wa Kenya Kwanza unaashiria watakuwa na mwelekeo mpya wa kisiasa 2027.

“Sasa tuko na Mudavadi, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangúla ndani ya serikali na wana nyadhifa muhimu. Sote tunaunga mkono utawala huu hata 2027,” akasema Bw Atwoli.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja naye alisisitiza kuwa kama jamii lazima waungane huku akiwakemea viongozi ambao wamekuwa wakivumisha miungano ya kikabila.

Aliposimama kuhutubu, Bw Mudavadi alimrejelea Rais kama kiongozi ambaye hana kisasi ndiposa akaamua kufanya kazi na hasimu wake Raila Odinga ambaye anawania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Aliposimama kuhutubu, Rais Ruto alionya dhidi ya siasa za kikabila huku akiahidi kuwa serikali yake itaipiga uchumi jeki na kutimiza ahadi iliyotoa kwa raia kuelekea uchaguzi wa 2022.

Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, wabunge Titus Khamala (Lurambi), Oscar Nabulindo (Matungu), Johnson Naicca (Mumias Magharibi) pia walihudhuria ibada hiyo.