Viongozi wakana Ruto anayeyusha ushawishi wa Uhuru Mlima Kenya
Na JOSEPH WANGUI
BAADHI ya viongozi wa kisiasa kutoka Mlima Kenya wametetea ziara za Naibu Rais William Ruto katika eneo hilo na kupinga vikali madai kwamba Bw Ruto amempiga kumbo Rais Uhuru Kenyatta kama kigogo wa siasa za uliokuwa mkoa wa kati.
Mwakilishi wa kike wa Nyeri Rahab Mukami, Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata na Mbunge wa Kirinyaga ya Kati Wambugu Munene wamekanusha vikali kwamba Rais Kenyatta hathaminiwi tena na wafuasi wake wanaosemekana kumkumbatia Bw Ruto anayeungwa mkono na viongzoi wengi waliochaguliwa.
“Bw Ruto hajachukua nafasi ya Rais Kenyatta kwasababu hii ni ngome ya chama cha Jubilee na yeye ndiye naibu kiongozi wa chama. Kwa kuwa tuko Jubilee tunamuunga mkono na tutazidi kushirikiana naye,” akasema Bi Mukami.
Aidha alisisitiza kwamba viongozi wanaoandamana na Naibu Rais katika ziara zake wanafanya hivyo kwa sababu za kimaendeleo wala si kisiasa.
“Bw Ruto huwa anapokelewa vyema na wananchi na si ukweli kwamba viongozi waliochaguliwa pekee ndiyo wanamuunga mkono. Kwa sasa ni bayana kwamba wananchi wa eneo hilo wanamuunga mkono Bw Ruto,” akaongeza Bi Mukami akisisitiza kwamba hakuna kilichobadilika akilini mwa wapiga kura tangu viongozi hao wawili walipofanya kampeni pamoja wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Kauli ya Bi Mukami iliungwa mkono na seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata aliyeunga hatua ya wabunge hao kuandamana na Bw Ruto ili kuhakikisha anamrithi Rais Kenyatta mwaka wa 2022 lakini akakanusha kwamba Rais Kenyatta hana ushawishi tena miongoni mwa wapiga kura.
“Wabunge hao walipiga hesabu zao na kuona kwamba njia ya kufuata inayoshabikiwa na wananchi ni kumuunga mkono Naibu Rais,” akasisitiza Bw Kang’ata.
Kuhusu madai kwamba Bw Ruto alivuruga uteuzi wa chama cha Jubilee mwaka uliopita ili kuhakikisha washirika wake ambao ni wabunge wa sasa walichaguliwa, seneta huyo alitaja madai hayo kama yasiyokuwa na msingi wala mashiko.
“Waliopoteza kura walikuwa wakitafuta visingizio ambapo ni jambo la kawaida katika siasa. Mtu kama Kabogo (gavana wa zamani wa Kiambu) hakupendwa na wananchi kutokana na uongozi wake wa kiimla. Ikiwa tutamlaumu Bw Ruto kwa hilo basi hatumtendei haki,” akaongeza Bw Kang’ata.
Mbunge wa Kirinyaga ya Kati Wambugu Munene hakutofautiana na wenzake na kuwakashifu wanaosema kwamba ziara za Bw Ruto eneo hilo ni njama ya kuanzisha kampeni mapema wakati wananchi wanafaa kupata huduma muhimu kutoka kwa serikali.
“Ikiwa nimeeleza nia yangu kuhusu mwaniaji ninayempigia upato mwaka wa 2022 hiyo si kampeni. Niko huru kufanya hivyo katika hafla yoyote. Bw Ruto tayari amejipendekeza kwa watu wa Mlima Kenya na hilo si baya kwa sababu bado anasaidia rais kufanya kazi kama makamu wake,” akasema Bw Munene.