Habari Mseto

Visa vya kutesa punda vyapungua Lamu mwezi Ramadhani

Na KALUME KAZUNGU March 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MATESO ambayo kwa kawaida punda hupitia katika kisiwa cha Lamu, yameripotiwa kupungua pakubwa wakati wa mwezi wa Ramadhani.

Imebainika kuwa, wamiliki wengi wa punda sasa wanawatunza vyema katika kipindi hiki huku pia kazi zikipungua kwa vile idadi kubwa ya wakazi ambao ni Waislamu, wamefunga biashara zao hadi mfungo ukamilike.

Takwimu kutoka Kituo cha Matibabu ya Punda Lamu zinaonyesha kuwa, visa kati ya 20 na 25 vya ukatili wa punda kupigwa na kujeruhiwa vilikuwa vikitokea kila siku.

Hata hivyo, tangu Ramadhani ianze, visa vimepungua zaidi ya nusu, ambapo ni vinane au 10 pekee vinavyoripotiwa.

“Msimu wa Ramadhani umeshuhudia hotuba zetu nyingi misikitini zikisisitizia waumini kuonyesha utu kwa viumbe vyote vilivyo hai vya Mungu. Ni vyema kwa wenye punda kuyashika haya. Isiwe tu nyakati za Ramadhani ndipo umtunze punda au mnyama wako. Kuwafanyia wanyama ukatili ni sababu tosha ya mtu kutupwa motoni,” akasema Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Kisiwani Lamu, Ustadh Abdulkadir Mau.

Bw Said Ahmed Kirume, mmiliki wa punda, alisema ni sehemu ya ibada kwa mja kutenda utu kwa wanyama.

“Mungu ameumba wanyama, wakiwemo punda na kuwafanya watiifu kwetu. Tunawategemea. Ni bora kuwaonyesha upendo, kushirikiana nao na kukimu mahitaji yao,” akasema Bw Kirume.

Bw Said Hussein, mmiliki mwingine wa punda, anasema Quran inadhihirisha umuhimu wa wanyama kwa binadamu.

Maafisa wa haki za wanyama kwenye kituo cha matibabu ya punda mjini Lamu walithibitisha ukatili dhidi ya punda umepungua mwezi huu.

Afisa wa Kushughulikia Matandiko ya Punda kituoni humo, Bw Amos Parsimei alisema visa vingi vya wanyama hao kuumizwa vinatokana na kubebeshwa mizigo mizito kupita kiasi na kukosa kuwekewa matandiko bora migongoni mwao.

“Tunaendeleza hamasa kwa wenyeji kuhakikisha punda wao wanatunzwa vyema wanapotekeleza majukumu ya kila siku,” akasema Bw Parsimei.

Daktari wa wanyama katika kituo hicho, Bw Obadiah Sing’oei, alisema wako mbioni kuzindua mpango utakaohusisha viongozi wa dini watakaoingia mashinani kuelimisha jamii kuhusiana na umuhimu wa kuheshimu haki za punda.

“Punda na mnyama mwingine yeyote ana haki ya kupewa chakula kizuri, maji, mahali pazuri pa kuishi, matibabu na tuepuke kuwapiga au kuwatesa. Ninafahamu kwamba Uislamu pia unazingatia haya kwa wanaotafuta thawabu mbinguni,” akasema Bw Sing’oei.