Vyama vya walimu vyaitaka TSC kuondoa walimu maeneo hatari
Na LEONARD ONYANGO
VYAMA vya walimu sasa vinataka Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kuondoa walimu wote kutoka maeneo ya Kaskazini Mashariki hadi serikali itakapowahakikishia usalama.
Chama cha Walimu wa Sekondari (Kuppet) na Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) Jumapili vilisema walimu katika ukanda wa Kaskazini Mashariki sasa wanahudumu kwa hofu kufuatia shambulio la kigaidi la Ijumaa ambapo walimu wawili wasiokuwa wenyeji waliuawa baada ya magaidi wa Al-Shabaab kuvamia shule ya Msingi ya Qarsa katika Kaunti ya Wajir.
Walimu hao Seth Oluoch Odada na Kevin Shari waliuawa wakiwa manyumbani mwao. Mkewe Odada, Caroline, pia aliuawa katika shambulio hilo lililotekelezwa alfajiri.
Viongozi wa Kuppet, waliokuwa wakihutubia wanahabari jijini Nairobi, walimshutumu Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kwa kusalia kimya tangu kutokea kwa shambulio hilo siku tatu zilizopita.
“Kufikia sasa Waziri wa Usalama hajatoa tamko lolote kuhusiana na shambulio hilo. Serikali imesalia kimya huku walimu wakichinjwa,” akasema Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori.
Alisema Kuppet itaitisha mgomo wa kitaifa endapo TSC itaadhibu walimu wanaotoroka Kaskazini Mashariki kwa sababu za kiusalama.
Kuondoa walimu
“Kufuatia shambulio hilo, chama cha Kuppet kinataka TSC kuondoa walimu wote kutoka Kaunti za Wajir na Mandera hadi watakapohakikishiwa usalama wao,” akasema Bw Misori.
Katika taarifa tofauti, Katibu Mkuu wa Knut Wilson Sossion alimtaka Waziri Matiang’i kubuni kikosi maalumu cha kulinda walimu na shule.
Alishutumu tume ya TSC kwa kuendelea kupuuza masilahi ya walimu na wanafunzi huku wakiendelea kuhangaishwa na magaidi.
Alisema kuwa walimu na wanafunzi wanasoma kwa hofu katika maeneo ya Wajir, Mandera, Garissa, Kerio Valley, Lamu na Tana River.
Mnamo 2015, walimu wasio wenyeji waligura maeneo ya Kaskazini Mashariki kufuatia shambulio la kigaidi.