Wachina waliochapa Mkenya mijeledi kuadhibiwa vikali na serikali
Na LEONARD ONYANGO
POLISI wamekamata raia wanne wa China kuhusiana na video iliyochipuka mtandaoni ikionyesha Mchina akichapa viboko Mkenya katika hoteli ya Chez Wou iliyoko mtaa wa Kileleshwa, Nairobi.
Maafisa kutoka Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) walisema kuwa Wachina hao walimakatwa baada ya kufanya uchunguzi kuhusiana na video hiyo ambayo imezua imewakera Wakenya.
Maafisa wa DCI walivamia hoteli hiyo jana na kuwanasa Deng Hailan, raia wa China ambaye anafanyakazi hotelini hapo, wapishi Chang Yueping, na Ou Qiang, na Yu Ling ambaye ni keshia.
Kulingana na DCI, Deng hana kibali cha kufanya kazi humu nchini.Chang Yueping na Ou Qiang wana viza zilizopitwa na wakati. Chang ana kibali cha kufanya kazi humu nchini lakini mwenzake hana, kwa mujibu wa DCI.
Yu Ling ambaye ni keshia ana viza ya wageni lakini hana kibali cha kufanya kazi humu nchini.“Kufuatia ripoti kuhusu mwanaume raia wa China aliyeonekana akimchapa mfanyakazi wa kiume, maafisa wa polisi kutoka Kituo cha Kilimani Jumapili walivamia hoteli ya Chez Wou mtaani Kileleshwa,” ikasema idara ya DCI.
Wakenya wanane wanaotekeleza majukumu mbalimbali hotelini hapo walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kilimani kuhojiwa.
Katika video hiyo, mwanaume wa Kichina anayeaminika kuwa Deng, anaonekana akiagiza Mkenya, anayedaiwa kuwa mhudumu hotelini hapo, kulala kifudifudi.
Mchina huyo amesimama kando huku akishikilia kiboko. Mwathiriwa analala chini na Mchina anamtandika viboko huku wenzake wakimtazama kutoka mbali.Mchina anasikika akimuuliza mwathiriwa sehemu ya mwili anayotaka kuchapwa.
Mkenya huyo alichapwa ubavuni na anaonekana akiwa mwenye maumivu. Mwathiriwa baadaye aliripoti dhuluma hizo katika Kituo cha Polisi cha Mlimani hivyo maafisa wa polisi wakaanzisha uchunguzi.Washukiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.
Mwaka jana, raia watatu wa China walikamatwa baada ya kupatikana wakiuza nyama ya mbwana wanyama wa porini kama vile kobe.
Washukiwa pia walikuwa na pembe za ndovu.Mnamo 2018, serikali ilimrejesha Mchina kwao baada ya kuwaita Wakenya nyani.
Mchina huyo Liu Jiaqi alitoa kauli hiyo ya ubaguzi wa rangi baada ya kuzozana na mmoja wa wafanyakazi katika kampuni moja iliyoko katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.