Habari Mseto

Wanaodaiwa kuua kasisi kushtakiwa kortini Embu

November 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA watatu wa mauaji ya Kasisi Michael Maingi Kyengo watashtakiwa kwa mauaji katika mahakama kuu ya Embu Jumatatu wiki ijayo.

Hakimu mkazi wa Mahakama ya Milimani Paul Mayova aliamuru polisi wawapeleke washukiwa hao kujibu mashtaka ya mauaji mbele ya Jaji wa Mahakama kuu kaunti ya Embu.

Bw Mayova alitoa agizo hilo baada ya kuombwa na kiongozi wa mashtaka ya umma awaruhusu maafisa wa polisi wawahoji washukiwa hao watatu kwa siku moja hadi leo ndipo wafunguliwe shtaka la mauaji.

“Kuna washukiwa watatu waliotiwa nguvuni kufuatia kifo cha Kasisi Kyengo aliyetoweka na maiti yake ikapatikana imezikwa katika ufuo wa mto kaunti ya Embu,” Bw Mayova alielezwa.

Hakimu alielezwa mshtakiwa polisi wanaochunguza kesi hiyo wamebakisha sehemu kidogo kukamilisha uchunguzi huo.

“Afisa anayechunguza kesi hii atasafiri hadi Embu kesho (leo) kukamilisha mahojiano na mashahidi kisha awafungulie washukiwa mashtaka katika mahakama kuu Embu,” mahakama iliambiwa.

Kiongozi huyo wa mashtaka alimweleza hakimu washukiwa wote Michael Mutunga, Mwangangi Kavivya na Solomon Mutava washtakiwa pamoja.

“Mutunga, Kavivya na Mutava watashtakiwa pamoja kwa mauaji ya Kasisi Michael Maingi Kyengo,” Bw Mayova alifahamishwa.

“Je mnapinga ombi mzuiliwe kwa siku moja zaidi kumwezesha afisa anayechunguza kesi dhidi yenu kusafiri hadi Embu kukamilisha uchunguzi?” Bw Mayova aliwauliza washukiwa.

“Hatupingi ombi hilo,” washukiwa walimjibu hakimu.Mahakama iliamuru washukiwa hao wazuiliwe hadi leo kumwezesha mkurugenzi wa mashtaka ya umma kuwafungulia mashtaka.

“Polisi watawasafirisha hadi Embu ambapo mtajibu shtaka la kumuua Kasisi Michael Kyengo,” Bw Mayova aliwaeleza washtakiwa.Hakimu aliamuru washukiwa hao wazuiliwe hadi Novemba 11 , 2019 watakapojibu shtaka la mauaji katika mahakama kuu ya Embu.

Wakili anayewatetea washukiwa hao hakupinga ombi hilo la kuwazuilia kwa siku moja ndipo afisi ya DPP iwafungulie mashtaka.

Mmoja wa washukiwa hao Kavivya wiki iliyopita alisimulia mbele ya hakimu mwandamizi Hellen Onkwani jinsi Kasisi Kyengo alivyouawa kinyama na maiti yake kuzikwa kando la mto.

Kavivya aliungama ni yeye alimfunga Kasisi Kyengo mikono na miguu akiwa uchi wa mnyama kisha wakamuua.

Mshukiwa huyo alikiri alilipwa Sh1,500 kumsaidia Mutunga kumuua aliyesema “walikuwa wanamtoa kafara.”

Hakufafanua ilikuwa kafara ya nini.Kasisi Kyengo alikuwa amefungiwa ndani ya buti la gari la Mutunga.Kasisi Kyengo alikuwa akihudumu katika kanisa la katoliki la Thatha kaunti ya Machakos.

Mara ya mwisho ya kuonekana akiwa hai ilikuwa Oktoba 8 2019 katika soko la Kaewa akiendesha gari lake.