Habari Mseto

Wanasiasa wakosa adabu mazikoni

December 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KITAVI MUTUA

WANASIASA mnamo Jumanne waligeuza mazishi ya Seneta Boniface Kabaka wa Machakos kuwa jukwaa la kurushiana cheche za matusi kuhusu siasa za ‘Handisheki’ na ‘Tangatanga’.

Viongozi kutoka mirengo yote ya kisiasa walielekezeana lawama na matusi mbele ya familia ya marehemu bila kujali hisia za waliofiwa, taswira iliyoonyesha mgawanyiko mkubwa wa kisiasa uliopo nchini kuhusiana na ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Familia ya marehemu na viongozi wa makanisa walionekana kukerwa lakini wasijue cha kufanya wakati wabunge na maseneta walipokiuka miito ya mratibu wa hafla kufupisha hotuba zao.

Siasa hizo zilianzishwa na aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko, aliyewalaumu maseneta kwa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata maagizo wanayopewa na aidha Rais Kenyatta, Bw Odinga na Naibu Rais William Ruto.

Bw Sonko aling’olewa mamlakani na Seneti wiki iliyopita, ambapo maseneta wa mrengo wa handisheki walipiga kura ya kumwondoa na wale wa Tangatanga wakapinga.

“Sina machungu kwa sababu mlining’oa mamlakani. Tayari, nimeenda mahakamani kupinga uamuzi huo. Yote nayaachia Mungu kwa sababu ninajua misukumo iliyowafanya kuniondoa uongozini,” akasema Bw Sonko.

Bw Sonko pia alidai kuwa atatoa video zinazoonyesha Bw Odinga na Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe wakimrai kushirikiana nao kwenye njama ya kumzima kisiasa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka. Alidai njama hizo zilihusu uchaguzi mdogo ulioisha juzi katika eneobunge la Msambweni, Kaunti ya Kwale.

“Nakwambia Bw Musyoka kuwa hawa watu wanakutumia tu kupata kura za kupitisha ripoti ya BBI. Baada ya hapo, hautakuwa kwenye mikakati yao ya siasa za 2022. Naomba kukutana nawe ili kukuonyesha hayo,” akasema Bw Sonko huku akishangiliwa na waombolezaji.

Baadaye, taharuki ilitanda Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria alipomtaja Bw Musyoka kama kiongozi ambaye hana maono, akidai kuwa Makamu Rais huyo wa zamani anaielekeza jamii ya Wakamba kwenye upinzani.

Kutokana na matamshi hayo, Seneta Enoch Wambua (Kitui) na mwenzake Mutula Kilonzo Junior (Makueni) walitishia kuagiza mbunge huyo atimuliwe kwenye hafla hiyo.

Hata hivyo, hafla iliendelea kwa saa kadhaa, huku zaidi ya maseneta 40 waliohudhuria wakitumia nafasi walizopewa kuzungumza kupigia debe mirengo yao ya kisiasa badala ya kumwomboleza marehemu.

Nao maseneta waaminifu kwa Dkt Ruto walitumia fursa hiyo kuhimiza ushirikiano wa kisiasa baina ya kinara wao na Bw Musyoka kwa ajili ya uchaguzi wa 2022.Maseneta hao Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Aaron Cheruiyot (Kericho), Samson Cheragei (Nandi), Christopeher Langat (Bomet) na Millicent Omanga (Maaum) walidai ushirikiano huo utasaidia jamii ya Wakamba kuingia serikalini.

Lakini Seneta Mutula aliwakemea akiwataja kama wanafiki: ‘Imekuwa vipi leo Kalonzo amekuwa muhimu kwa mipango ya Ruto?

Hali ilipozidi, ilibidi Gavana Alfred Mutua (Machakos) kuingilia kati na kuchukua udhibiti wa hafla hiyo, akisema ilisikitisha hotuba ndefu za wanasiasa zilikuwa zikichelewesha mazishi ya marehemu na kuilazimu familia kumzika kwa giza.

Imekuwa kawaida kwa wanasiasa nchini kutowaheshimu walioaga wala familia zao, na badala yake hutumia mazishi kama majukwaa ya kujipigia debe badala ya kuomboleza.