Habari Mseto

Waziri wa Kilimo: Ni aibu kwamba tunatumia Sh520 bilioni kuagiza chakula ng’ambo

Na GEORGE MUNENE October 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KENYA hutumia Sh520 bilioni kila mwaka kuagiza chakula kutoka nje, kulingana na Waziri wa Kilimo Andrew Karanja.

Baadhi ya bidhaa za chakula zinazoagizwa kutoka ng’ambo ni pamoja na mchele, mafuta ya kupikia na ngano.

Kwa mfano, inakadiriwa kuwa zaidi ya tani milioni moja za mchele huagizwa kila mwaka kutoka nchi za ng’ambo.

Dkt Karanja alisema ni aibu kwamba nchi kama Kenya yenye uwezo wa kuzalisha chakula inatumia fedha nyingi kununua chakula kutoka ng’ambo.

“Ninaaibika kama Waziri wa Kilimo kupewa takwimu hizo,” akasema.

Akiongea mnamo Jumamosi katika eneo la Mutithi, Kaunti ya Kirinyaga alipofungua rasmi maonyesho kuhusu aina mbalimbali za teknolojia ya kilimo, maarufu kama Agitech 2024 Exposition, Dkt Karanja alikariri kuwa Kenya iko na uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosheleza idadi ya watu inayoendelea kuongezeka kila siku.

“Ni wajibu wetu, haswa sekta ya kibinafsi kuwekeza katika uzalishaji wa chakula ili tukome kutegemea vyakula vinavyoagizwa kutoka nje,” akasema.

Waziri Karanja alisisitiza kuwa serikali iko tayari kufanyakazi na sekta ya kibinafsi “kupunguza kiwango cha fedha zinazotumika kununua chakula kutoka ng’ambo.”

“Afisi yangu itakuwa wazi kwa mtu yeyote ambaye anataka kukodisha shamba kutoka kwa serikali ili aweze kuwekeza katika miradi ya kilimo. Tufanye kazi pamoja kushughulikia suala hilo na kutegemea chakula kutoka ng’ambo,” akasema.

Dkt Karanja, ambaye alikuwa ameandamana na mwenyekiti wa Kampuni ya Kutengeneza Mbegu Nchini (KSC), alisema serikali inapanga kupanua maeneo ya kutumika kwa kilimo cha unyunyiziaji ili kuongeza uzalishaji wa chakula.

Alisema kuna mbegu za kutosha kwa msimu huu wa upanzi na akawataka wakulima kununua mbegu hizo kutoka kwa wauzaji walioidhinishwa.