Habari Mseto

Wezi waliopiga kambi nyumbani kwa bwenyenye kwa wiki moja wanyakwa

March 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na KITAVI MUTUA

WAKAZI wa mji wa Matuu, Kaunti ya Machakos, wameshangazwa na wezi ambao walipiga kambi kwa wiki moja katika boma la mfanyabiashara wa eneo hilo wakipika, kula, kustarehe, kuvua samaki na kisha kuiba mali yake.

Genge hilo la wezi kumi liliwashangaza maafisa wa polisi na majirani wa Bw Michael Matheka kwa ujasiri wao wa kuishi katika nyumba yake kwa wiki moja, wakistarehe, kutazama televisheni, kulala na kuiba vyombo vya nyumbani bila wasiwasi.

Inashukiwa kuwa wezi hao walikuwa wakishinda katika boma la Bw Matheka mchana na kubeba mali yake usiku kabla ya kurejea tena alfajiri kuendelea kustarehe.

Polisi wanasema kwamba wakati wa mchana, washukiwa hao walikuwa wakivua samaki kutoka kidimbwi kilichoko katika boma la mfanyabiashara huyo na kuwatumia kujiandalia kitoweo walichokula kwa ugali.

Wezi hao walikuwa wamefuatilia mienedo ya Bw Matheka ambaye ana duka la kuuza vifaa vya stima mjini Wote, kaunti ya Makueni na kubaini kwamba hangefika nyumbani kwa siku kadhaa.

Kulingana na Bw Matheka, waliingia katika nyumba yake kwa kutumia ngazi kupanda ua unaozunguka boma lake ambayo walifungua mlango ulio orofa ya kwanza kwa ufunguo maalamu.

Kulingana na Bw Matheka, wezi hao waliburudika kwa mvinyo uliokuwa nyumbani kwake bila kushukiwa na majirani.

Wiki moja kabla ya kisa hicho, Bw Matheka alikuwa amehusika katika ajali ya barabarani mjini Tawa, eneo la Mbooni ambapo mtu mmoja anayemfahamu alikufa na ikabidi asiondoke Makueni wakiandaa mazishi.

“Inaonekana walijua mimi na familia yangu hatungekuwa nyumbani kwa sababu waliishi katika nyumba yangu bila wasiwasi wa kukamatwa,” alisema na kuongeza kuwa kwa kawaida wezi hutumia muda mfupi kuiba.

Mwanzoni, majirani walidhani washukiwa walikuwa jamaa za Bw Matheka ambao waliomtembelea hadi walipoanza kuwaona wakibeba vyombo vya elektroniki, godoro na vifaa vingine. Ni wakati huo ambapo walimfahamisha Bw Matheka na polisi ambao walivamia nyumba hiyo Ijumaa alasiri.

Ajabu ni kwamba nyumba hiyo iko kilomita moja kutoka kituo cha polisi cha Matuu.

Washukiwa hao waliruka kupitia ukuta na kutoroka baada ya polisi kufyatua risasi hewani lakini wakazi waliwafuata na kuwakamata wakitisha kuwachoma. Mkuu wa polisi eneo la Matuu Bw Edward Kipsang Changach alisema polisi waliwakamata washukiwa wanne na wanawasaka sita waliotoroka.

Afisa wa jeshi aliyetajwa na mshukiwa mmoja kwenye mahojiano pia anatafutwa lakini hakuwa katika nyumba hiyo polisi walipoivamia. Bw Changach alisema walipata vyombo vya thamani ya Sh650,000 zilizoibwa kutoka nyumba hiyo.

Kwingineko, polisi mjini Eldoret jana walimtia nguvuni mtu anayeshukiwa kuhusika katika mauaji ya afisa wa polisi wa utawala.

Isaac Nyairo Ondora maarufu kama ‘Kaloki’, alikamatwa mtaani Langas kuhusiana na kuuawa kwa polisi wa Utawala Joseph Kilunda Ndinda, aliyekuwa akihudumu katika chuo cha ufundi cha kitaifa cha Eldoret.

Mwili wa marehemu ulipatikana ukiwa umetupwa katika barabara kuu ya Eldoret –Kapsabet karibu na mtaa wa Langas mnamo Machi 4.

Kisa hicho kilithibitishwa na afisa mkuu wa polisi katika eneo la Eldoret Kusini, Bw Waqo Abduba, aliyesema maafisa wake wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo.

Hata hivyo polisi wanashuku huenda marehemu aliuawa mahali tafauti kabla ya mwili wake kutupwa kando ya barabara kuu ya Eldoret – Kapsabet.

Mshukiwa alifikishwa mahakamani hapo jana lakini hakuruhusiwa kujibu mashtaka hadi pale atakapofanyiwa uchunguzi wa kiakili.

Kesi hiyo itatajwa Machi 15 mwaka huu.

Habari za ziada na TITUS OMINDE