Askofu aitaka NASA ikubali Uhuru Kenyatta ni Rais halali
Na SAMMY LUTTA na VALENTINE OBARA
Kwa Muhtasari:
- Askofu Sapit asema kipindi cha kampeni kilikamilika 2017 na nchi inahitaji utulivu
- Awataka Wakenya kusubiri hadi 2022 uchaguzi mwingine wa urais utakapoandaliwa
- Mashauriano ya kisiasa yanafaa yawe kuhusu jinsi sheria za uchaguzi zinaweza kurekebishwa
- Kiongozi huyo aonya Kenya itabaki nyuma kimaendeleo na kiuchumi hali ya kisiasa nchini ikizidi kushuhudiwa
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana la Kenya (ACK), Bw Jackson ole Sapit, Jumatatu alisema Muungano wa NASA unafaa kusubiri hadi mwaka wa 2022 ili ushiriki kwenye uchaguzi wa urais kwani Rais Uhuru Kenyatta yuko mamlakani kihalali.
Askofu Sapit alisema kipindi cha uchaguzi kilikamilika 2017 na nchi inahitaji utulivu ili kuleta maendeleo na huduma kwa wananchi baada ya serikali kuundwa.
“Tunahitaji kukomesha siasa na tusubiri hadi 2022 kwani wakati huyo ndio viti vya kisiasa vitakuwa wazi kikatiba na wale wanaotaka kuwa wagombeaji wataruhusiwa. Ninaomba walio serikalini na katika upande wa upinzani washauriane kuhusu jinsi ya kuleta umoja kwa Wakenya ambao kwa sasa wamegawanyika kisiasa,” akasema.
Alikuwa akizungumza na wanahabari katika kanisa la St Paul’s ACK, parokia ya Lodwar baada ya kuzindua lango jipya na maduka yaliyojengwa.
Uchumi utayumba
Kiongozi huyo wa kidini alisema Kenya itabaki nyuma kimaendeleo na kiuchumi kama hali ya kisiasa itazidi kushuhudiwa kwa muda mrefu huku upande wa upinzani ukitaka mmoja wao awe rais.
Alisema kanisa linaomba kila mmoja nchini akumbatie uwiano na uvumilivu wa kisiasa ili kuwe na amani huku akiongeza kuwa serikali iliyopo inafaa kuwa katika mstari wa mbele kueneza umoja wa kitaifa.
Bw Sapit alisema mashauriano ya kisiasa yanafaa yawe kuhusu jinsi sheria za uchaguzi zinaweza kurekebishwa ili kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa 2022 utafanywa kwa njia bora zaidi.
“Hatuhitaji mashauriano kuhusu jinsi Kenya inaweza kupata rais mpya hivi sasa kwa kuwa nchi tayari ina Rais Uhuru ambaye aliapishwa mamlakani baada ya ushindi wake kukubaliwa na Mahakama ya Juu,” akasema na kusisitiza kuwa nchi haiwezi kuwa na marais wawili kwa wakati mmoja.
Msimamo sawa na mabalozi
Msimamo wake ni sawa na uliotolewa na mabalozi wa nchi za magharibi ambao walimtaka Bw Odinga atambue uhalali wa uongozi uliopo kabla kuwe na mashauriano kuhusu mabadiliko anayotaka.
Bw Odinga alikashifu mabalozi hao 11 na kusema hawana haki ya kuamulia wananchi wa Kenya kuhusu uongozi wanaotaka kwani walionyesha ubaguzi wao wakati wa uchaguzi wa urais mwaka uliopita.
Mshauri wa kiongozi huyo wa Chama cha ODM, Bw Salim Lone, pia alikosoa mabalozi hao na kusema msimamo wao unaweza kufanya pande zote mbili zizidi kuwa na misimamo mikali.
Kulingana naye, Bw Odinga amekuwa mvumilivu kwa muda mrefu na hata aliepuka wito wa wafuasi wake mara nyingi walipomtaka ajiapishe kuwa rais, na hatimaye akajiapisha tu kuwa ‘rais wa wananchi’ na wala si wa Jamhuri ya Kenya.