Habari za Kitaifa

Chama cha Jubilee chaanza kampeni za Matiang’i kumenyana na Ruto 2027

Na WINNIE ATIENO April 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha Jubilee cha Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kimeanza kumtafutia aliyekuwa Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i umaarufu eneo la Pwani.

Chama hicho kilichounda serikali iliyopita kimemchagua Dkt Matiang’i kupeperusha bendera yao kama mgombea wa Urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Jeremiah Kioni alisema wameanza kumpigia debe mgombea wao eneo la Pwani. Alisema mgombeaji wao ndiye atakayekomboa taifa hili dhidi ya uchumi uliozorota.

Akiongea hapo Jumanne, Aprili 1, 2025, kwenye hafla maalum eneo la Nyali, Bw Kioni na Naibu Katibu wa chama hicho Bw Yasir Noor waliwasihi Wakenya kuunga mkono mgombea wao.

“Tumeshatangaza nahodha wetu ambaye ni Dkt Matiang’i ambaye tuna imani atabadilisha nchi hii siku 100 baada ya kuapishwa. Serikali ya Kenya Kwanza imewahadaa Wakenya ambao sasa wanahangaika,” alisema Bw Kioni.

Alisema wamepata uungwaji mkono kutoka kwa kinara wao Bw Kenyatta kando na wakazi wa Mlima Kenya.

“Wakazi wote wa Mlima Kenya wanaunga mkono mgombea wetu sasa tumefika hapa baharini kusaka uungwaji mkono,” alisema Bw Kioni.

Alisema chama hicho kililemazwa baada ya kushtakiwa kupitia misukosuko mingi na kushindwa kupanga mikakati yao kikamilifu.

Hata hivyo, Bw Kioni alisema wametamatisha kesi zao walizoshinda mahakamani na kuchukua usukani wa chama hicho.

Alisema wameanza kampeni za mapema na kusaka wanachama na kuuza sera sehemu zote nchini kando na kufungua afisi zao.

“Nimewahakikishia wakuu wa chama chetu, wagombea na wanachama wote kwamba hatutamezwa na chama chochote, tutasalia Jubilee na kugombea viti vyote nchini,” aliongeza.

Bw Kioni alisema chama hicho kitawapa kipaumbele wale ambao walisimama kidete na Jubilee ili wapeperushe bendera yao.

“Uteuzi wetu utakuwa wa haki na usawa, lakini tutawazawadi wale ambao walisimama kidete na chama chetu. Wale ambao waliamua kusimama na sisi licha ya kuhadaiwa na mapochopocho ili kujiunga na vyama vingine ndio watakaofaidi,” alisema Bw Kioni.

Bw Noor alimsifu Bw Kenyatta kwa misingi bora ya miradi ya maendeleo nchini aliyoanzisha alipokuwa mamlakani.