FKE yapata Rais wa kwanza mwanamke
NA JAEL MAUNDA
MSOMI Dkt Gilda Odera ndiye mwanamke wa kwanza kuwa rais wa Shirikisho la Waajiri Nchini Kenya (FKE) baada ya kuchaguliwa katika makala ya 65 ya Mkutano Mkuu wa Mwaka mnamo Jumatano.
Dkt Odera alichaguliwa katika uchaguzi uliofanyika katika hoteli ya JW Mariott jijini Nairobi Jumatano.
Anachukua usukani kutoka kwa Dkt Habil Olaka aliyehudumu kwa kipindi cha miaka miwili.
Kabla ya kuchaguliwa kuongoza shirikisho hilo, Dkt Odera alikuwa naibu wa kwanza wa rais katika FKE kwa miaka miwili iliyopita.
“Ninaahidi kushirikiana na serikali iliyoko mamlakani kwa nia moja tu ya kutimiza malengo ya FKE,” akasema Dkt Odera.
Naibu wake wa kwanza katika FKE ni Bw Mike Macharia naye Bw Laurence Okelo alichaguliwa naibu wa pili.