Habari za Kitaifa

ILIKUWA MTEREMKO: Kindiki, Joho, Murkomen na wenzao 16 kujaajaa afisini kwa bashasha

Na CHARLES WASONGA August 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAWAZIRI wapya 19 sasa wataingia afisini Alhamisi Agosti 8, 2024 baada ya kuapishwa rasmi katika sherehe itakayoongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Kulingana na taarifa fupi iliyotolewa Jumatano jioni na katibu wa kitengo cha habari za ikulu Emmanuel Tallam, shughuli hiyo itaanza saa tatu asubuhi.

Mawaziri hao wateule wataapishwa siku moja tu baada ya wao kuidhinishwa na wabunge walipopitisha ripoti ya Kamati ya Uteuzi iliyopendekeza wateuliwe rasmi kushikilia nyadhifa husika.

Hata hivyo, ndoto ya Bi Stella Soi Lang’at ya kuhudumu kama Waziri wa Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi ilizimwa na Kamati hiyo iliyoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ilipokataa uteuzi wake.

Akiwasilisha ripoti ya shughuli ya kamati hiyo bunge, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah alisema hakudhihirisha uelewa wake wa masuala yanayohusu wizara hiyo.

“Bi Lang’at, ambaye ni mtumishi wa umma mwenye uzoefu mkubwa, hakudhihirisha uelewa na masuala yanayohusu Wizara ya Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi. Hii ndio maana kamati ilikosa kumwidhinisha kwa wadhifa huo. Tunamwomba Rais ampendekeze kwa wadhifa mwingine serikali na ateue mtu mwenye ufahamu mpana wa majukumu ya wizara hii muhimu,” akaongeza Mbunge huyo wa Kikuyu.

Wafuatao ndio watakaoapishwa Alhamisi; Profesa Kithure Kindiki atakayeapishwa kama Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Debra Barasa (Waziri wa Afya), Alice Wahome (Waziri wa Ardhi), Julius Migos (Waziri wa Elimu), Soipan Tuya (Waziri wa Ulinzi) na Eric Muuga (Waziri wa Maji).

Wengine ni pamoja na; Aden Duale ambaye atalishwa kiapo kuhudumu kama Waziri wa Mazingira, Davis Chirchir (Waziri wa Barabara), Margaret Nyambura (Waziri wa ICT), John Mbadi (Waziri wa Fedha), Salimu Mvurya (Waziri wa Biashara), Rebecca Miano (Waziri wa Utalii), Opiyo Wandayi (Waziri wa Kawi), Kipchumba Murkomen (Waziri wa Michezo), Ali Hassan Joho (Waziri wa Uchumi wa Majini), Alfred Mutua (Waziri wa Leba), Wycliffe Oparanya (Waziri wa Ustawi wa Vyama vya Ushirika) na Justin Muturi (Waziri wa Utumishi wa Umma).

Kumi kati ya hawa ni mawaziri walioteuliwa upya na Rais Ruto baada ya kuwafuta kazi mawaziri wote mnamo Julai 11, 2024, isipokuwa Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

Watano kati yao ni wataalamu katika nyanja mbalimbali huku wanne wakiwa wanachama wa ODM ambao Rais aliamua kuwajumuisha katika baraza lake la mawaziri kuunda kile alichokitaka kama Serikali Jumuishi.

Wao ni John Mbadi, Wycliffe Oparanya, Ali Hassan Joho na James Opiyo Wandayi.

Mnamo Jumatano, jioni Spika Wetang’ula aliwaagiza Mabw Wandayi (ambaye amekuwa akihudumu kama Mbunge wa Ugunja) na Bw Mbadi ambaye amekuwa akihudumu kama Mbunge Maalum, kujiuzulu rasmi nyadhifa zao kwa kuwasilisha barua afisini mwake.

Hii ni kwa sababu kulingana na kipengele cha 152 (4) cha Katiba wabunge watakaoteuliwa na Rais kuwa mawaziri sharti wajiuzulu baada ya uteuzi wao kuidhinishwa na Bunge.