Jumwa: Rais akiona anirudishe uwaziri nitashukuru, akiona ateue Joho ni sawa pia
ALIYEKUWA Waziri wa Jinsia na Utamaduni, Bi Aisha Jumwa amesema hahitaji kupigiwa debe, kufanyiwa kampeni wala kutetewa na wanasiasa ili ateuliwe tena kwenye baraza la mawaziri katika serikali ya Kenya Kwanza.
Akiongea kwa mara ya kwanza tangu afutwe kazi pamoja na mawaziri wenzake wiki iliyopita, Bi Jumwa alisema atamuunga mkono Rais Ruto iwapo atamchagua aliyekuwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho kwenye baraza lake la mawaziri.
“Sihitaji kutetea wala kupigiwa debe ili niteuliwe tena kwenye baraza la mawaziri, Rais ananijua na akiona vyema kunirejesha kazini nitashukuru na pia akiniambia nipumzike bado nitamshukuru,” alisema Bi Jumwa.
Bi Jumwa ambaye alikuwa mstari wa mbele kumpigia debe Dkt Ruto kwenye kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu wa 2022, alimshukuru Rais kwa kumteua kwenye baraza la mawaziri.
Akiongea na Taifa Leo, Bi Jumwa alisema anaunga mkono serikali ya muungano ambayo itapesababisha kuchaguliwa kwa baadhi ya viongozi wa upinzani serikalini.
“Ikiwa Rais atamchagua Bw Joho kwenye baraza la mawaziri nitamuunga mkono. Nilienda Kilifi Jumamosi na nikaungana na wakazi ambao pia walishangilia ujumbe wangu wa kumshukuru Rais,” alisema Bi Jumwa.
Alisema aliamua kupasua mbarika baada ya kuona watu wakimfanyia kampeni arudishwe kazini.
Hata hivyo, aliwataka wale ambao wanampigia debe kumpa Rais Ruto muda na amani kwa kusaka baraza lililosalia.
“Msinipigie debe, Rais ananijua,” akasema Bi Jumwa. Kuelekea kura ya 2022, Bi Jumwa alihama chama cha ODM na kujiunga na UDA, kumpigia debe Dkt Ruto.
Alipoulizwa hatua atakayoichukua endapo hatochaguliwa Bi Jumwa alisema bado ni mapema sana kutoa uamuzi huo.
“Tumsubiri Rais amalize uteuzi wa baraza lake la mawaziri. Lakini akimchagua Bw Joho nitampongeza sababu serikali ya muungano ndiyo tunayoitaka),” aliongeza mwanasiasa huyo.
Mwenzake ambaye alifutwa kazi Bw Salim Mvurya naye amesalia kimya tangu kubanduliwa aliahidi kutoa maoni yake baadaye.
“Niko kwenye mkutano, nitazungumza baadaye,” alisema Bw Mvurya.
Bw Mvurya amekuwa akinyemelea kurithi nafasi ya Bw Joho katika siasa za Pwani baada ya kutoweka kwenye siasa za kitaifa kwa muda baada ya uchaguzi mkuu wa 2022. Hata hivyo ujio wa Bw Joho kulisambaratisha azma yake.
Bi Jumwa na Bw Mvurya ni mojawapo ya mawaziri waliosimamishwa kazi mnamo Julai 11, 2024, kufuatia maandamano ya vijana nchini.
Rais Ruto alisema atashirikiana na wanasiasa wengine katika kuunda baraza lake.
Julai 19, 2024, Rais alitaja baraza lake jipya na kuwaregesha mawaziri sita aliowafuta wakiwemo Prof Kithure Kindiki (Usalama), Bi Soipan Tuiya (Mazingira), Bi Alice Wahome (Ardhi), Davis Chirchir (Uchukuzi) na Aden Duale (Ulinzi).