Kalonzo atetea makanisa, aomba viongozi wa kidini waombee serikali ya Kenya Kwanza
KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amekashifu serikali ya Kenya Kwanza kwa kuibua mgogoro na viongozi wa kidini kuhusiana na misimamo yao ya visa vya ufisadi na maadili.
Viongozi wa kidini wamekuwa na msimamo thabiti kuhusu utaratibu wa wanasiasa kutoa sadaka na michango makanisani.
Akiandamana na mwenzake wa DAP-K Eugene Wamalwa katika ibada kanisani jijini Nakuru, Bw Musyoka alisema kanisa limetoa mwelekeo wa uongozi wa nchi kisheria na kiungu.
“Rais William Ruto anafaa kusikiliza kanisa kwa sababu Mungu anazungumza kupitia watu aliowatawaza,” akasema.
“Kanisa linafaa kutuombea tuwe na ujasiri kama ule wa maaskofu wa katoliki kwa kupinga siasa za utengano, uongo na ukabila ambazo zimegawanya nchi,” akaongeza Bw Musyoka akikashifu serikali kwa kukithiri kwa visa vya utekaji nyara nchini.
Makamu wa rais wa zamani aliandamana na aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, Seneta wa Kitui Enock Wambua na madiwani kadhaa wa eneo la Ukambani.
Wote walihudhuria ibada katika kanisa la St Joseph the Worker Parish eneo la Racecourse.
Bw Musyoka alitoa changamoto kwa viongozi serikalini akiwataka wafikirie kwanza kuhusu Wakenya kabla ya kufanya uamuzi wowote.
Alisisitiza kuwa hakuna nafasi za ulaghai wa kisiasa nchini.
“Ombeeni viongozi wa Kenya Kwanza ambao wana roho mbaya sana, roho ya utekaji nyara. Yaani, mtu anamteka mwenzake nyara, anamweka ndani ya Subaru, anakimbizwa na kutembezwa kila mahali nchini… Wanaowateka nyara ni Wakenya, wanabeba bunduki ambazo zimenunuliwa na ushuru wa wananchi wa Kenya. Tuombe huyo shetani aondoke Kenya,” aliendelea.
Kauli yake ilirejelewa na Bw Wamalwa ambaye aliwaunga mkono viongozi wa kidini kuhusiana na msimamo wao dhidi ya ufisadi.
“Iwapo umekuwa ukiwadanganya Wakenya, katika uchaguzi ujao, Wakenya watawapinga viongozi waongo ambao wamekuwa wakijihusisha na ufisadi,” akasema Bw Wamalwa.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan