Habari za Kitaifa

Kanja aapa kukabili wahuni wanaolipwa na wanasiasa kuzua fujo

Na MERCY MWENDE April 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

INSPEKTA Jenerali wa Polisi , Douglas Kanja, ameapa kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaokodiwa na wanasiasa kuvuruga shughuli za umma, kufuatia visa vya hivi majuzi vya vurugu katika kaunti za Kirinyaga na Nairobi.

Akizungumza na wanahabari wakati wa uzinduzi wa gari jipya la polisi katika Kituo cha Polisi cha Endarasha, Kaunti ya Nyeri, Bw Kanja alilaani vikali ghasia hizo na kusisitiza kwamba yeyote atakayehusika – bila kujali chama au msimamo wa kisiasa – atakabiliwa na mkono wa sheria.

Onyo hilo kali lilitolewa Jumatano baada ya wafuasi wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na mpinzani wake wa kisiasa, mbunge wa Mathira Eric  Wamumbi, kukabiliana wakati wa mazishi ya kiongozi wa kwaya, Bi Muchiru Mumbuchi, katika kijiji cha Muragara, Eneo Bunge la Ndia.

Mazishi hayo yalivurugwa na kusababisha hofu miongoni mwa waombolezaji waliolazimika kutawanyika kwa haraka, na shughuli kusitishwa ghafla.

“Katika Kirinyaga, tutawakamata wote waliohusika na kuwapeleka mahakamani,” alisema Bw Kanja. “Wahalifu wote watakabiliwa kisheria mahakamani na kujibu mashtaka yao.”

Bw  Kanja aliongeza kuwa polisi hawatavumilia tena uhalifu wa kisiasa unaochochewa na viongozi wenye tamaa ya mamlaka.

“Hatutakubali wahuni. Mtu yeyote anayevunja sheria — iwe ni mhalifu wa kawaida au mfuasi wa mrengo wa kisiasa — atakabiliwa na sheria bila mapendeleo,” aliongeza kwa msisitizo.

Kauli yake ilijiri siku chache baada ya vurugu kutokea Jumapili, Aprili 6, katika Kanisa la PCEA Mwiki, eneo la Kasarani, Nairobi.

Katika tukio hilo, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, aliyehudhuria ibada kanisani humo, alilazimika kujificha baada ya kundi la vijana wenye silaha kuvamia kanisa hilo na kuwatia hofu waumini.

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa washambuliaji hao waliwasili kwa pikipiki na inadaiwa walikuwa wameajiriwa kuvuruga ibada hiyo.

Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Uhalifu  (DCI) ameanzisha uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo, ambao IG Kanja amesema unakaribia kukamilika.