Kaunti nane zaanikwa kwa kuajiri wafanyakazi kinyume cha sheria
SERIKALI nane za Kaunti ziliajiri maelfu ya wafanyakazi bila kufuata sheria katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024, ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, imefichua.
Kulingana na ripoti hiyo, wafanyakazi hao waliajiriwa pasina nafasi za ajira kutangazwa kupitia vyombo vya habari na mahojiano kufanywa.
Ufichuzi huo katika ripoti ya hivi punde iliyotolewa wiki jana unaonyesha kuwa wafanyakazi hao walioajiriwa katika kaunti za Samburu, Trans Nzoia, Nairobi, Narok, Nandi, Embu, Machakos na Uasin Gishu wanaendelea kulipwa mamilioni ya fedha kama mishahara na marupurupu kila mwezi.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa katika kaunti zingine, hakukuwa na ushahidi kuwa nafasi wazi za ajira zilikuwepo kabla ya wafanyakazi wapya kuajiriwa.
Na katika kaunti zingine, faili zenye maelezo kuhusu uajiri wa wafanyakazi wapya hazikuwepo.
Wafanyakazi walioajiriwa kwa njia hiyo isiyozingatia sheria ni pamoja na maafisa wa usimamizi, walimu wa chekechea, makarani, wakurugenzi wa idara mbalimbali, maafisa wa ustawi wa kibiashara na maafisa wa kitengo cha usalama.
Kwa mfano, katika Kaunti ya Samburu, serikali hiyo iliajiri watu 29 kufanya kazi katika Kitengo cha Utekelezaji Miradi katika Afisi ya Gavana bila idhini kutoka kwa Bodi ya Uajiri wa Watumishi wa Umma katika Kaunti (CPSB).
Ndani ya kipindi hicho cha ukaguzi wa matumizi ya fedha za umma katika kaunti, hamna rekodi kuhusu matangazo ya nafasi za kazi, uorodheshaji wao baada ya mchujo, mahojiano na uteuzi kamili ziliwasilishwa kwa wakaguzi.
“Kufikia wakati huo wafanyakazi 29 walikuwa wamelipwa jumla ya Sh60 milioni na Kaunti ya Samburu. Isitoshe, kitengo cha utekelezaji miradi katika Afisi ya Gavana ambako walikuwa wakihudumu kwa mfumo wa utawala katika Kaunti ya Samburu. Majukumu ya wafanyakazi hao pia hayakuelezwa,” kulingana na ripoti hiyo ya Bi Gathungu.
“Hii ni kinyume na hitaji la Sehemu ya 68 ya Sheria za Serikali ya Kaunti ya 2012 inayohitaji kuwa bodi ya CPSB ihifadhi rekodi ya watu wote waliotuma maombi ya ajira na yapokelewe baada ya nafasi za ajira kutangazwa na rekodi hizo kufanyiwa ukaguzi kuhakikisha kuwa ni sahihi,” ripoti hiyo ikaeleza.
Isitoshe, ilibainika kuwa Gavana Jonathan Lati Lelelit wa Samburu alibuni kitengo hicho wakati ambapo bodi ya CPSB haikuwepo kwani muhula wa kuhudumu kwa wanachama wa zamani ulikuwa umekamilika.
Tayari kamati moja ya Seneti imeamuru kwamba Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) iingilie kati na kuamua kuwa Kitengo cha Utekelezaji Miradi katika Afisi ya Gavana ni batili na maafisa wote waliojiriwa huku walazimishwe kurejesha pesa zote walizolipwa kama mishahara kwani waliajiriwa kinyume cha sheria.
“Kwa kuwa hamna ushahidi kuwa bodi ya CPSB ilishauriwa, tunaamuru kwamba EACC iagize kwamba pesa zilizolipwa maafisa walioajiriwa katika kitengo hicho, kama mishahara na marupurupu zirejeshwe. Huu ni ukiukaji wa sheria,” akasema Seneta Moses Kajwang’ ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma katika Kaunti.
Katika Kaunti ya Narok, makarani 73, maafisa 27 wa utekelezaji wa maendeleo ya biashara na maafisa wawili wa utawala waliajiriwa kinyume cha sheria.
Jijini Nairobi, serikali ya kaunti iliajiri wafanyikazi 3,834 bila kufuata utaratibu unaofaa.
Ukaguzi unaonyesha kuwa hakuna tangazo lililotolewa kwa nafasi hizo na orodha za mchujo hazikufanyika wakati wa mchakato wa uajiri.Huko Embu, kaunti iliajiri wafanyikazi 911 katika nyadhifa mbalimbali kinyume cha sheria.
Katika Kaunti ya Trans Nzoia, rekodi za wafanyakazi zilifichua kuwa Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti iliwaajiri maafisa 258 katika nyadhifa mbalimbali lakini hakukuwa na ushahidi wa tangazo la nafasi za kazi.
Huko Nandi, jumla ya Sh6.5 milioni zilitumwa kama mshahara kwa wafanyakazi 139 ambao faili zao za kibinafsi hazikuwa na barua zao za kuteuliwa, sifa za masomo na rekodi zingine za ajira.
Katika Kaunti ya Uasin Gishu, wafanyakazi 181, wakiwemo walimu wa chekechea waliajiriwa bila kufuata utaratibu.