Habari za Kitaifa

Kenya yatarajia kuzalisha magunia milioni 70 ya mahindi na kuwashinda Tanzania na Uganda

Na VITALIS KIMUTAI August 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UZALISHAJI wa mahindi nchini unatarajiwa kupanda hadi magunia milioni 70 mwaka huu kutokana mikakati mwafaka ya kuinua sekta ya kilimo iliyowekwa na serikali.

Baadhi ya mikakati hiyo ni mbolea ya ruzuku na mvua nyingi, huku maeneo ya Bonde la Ufa na Magharibi mwa Kenya yakiibuka kuwa ngome kuu ya uzalishaji wa chakula.

Katibu katika Wizara ya Kilimo, Dkt Paul Kipronoh Ronoh alitangaza kuwa serikali imenunua magunia milioni 2.5 ya mbolea ya kuuzwa kwa wakulima chini ya mpango wa ruzuku kwa msimu ujao.

“Uzalishaji wa mahindi ulipanda hadi magunia milioni 67 msimu uliopita ikilinganishwa na magunia milioni 44 msimu uliotangulia.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya magunia milioni 70 yatazalishwa mwaka huu na wakulima,” Dkt Ronoh alisema.

“Hatua zilizowekwa na serikali zimeshuhudia kupanda kwa uzalishaji kwa magunia milioni 23 ya mahindi katika miaka miwili, na tunatarajia ongezeko zaidi la angalau magunia milioni tatu msimu huu wa mavuno.”

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, serikali iliuza magunia milioni 8.5 ya mbolea ya ruzuku kupitia maduka ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kwa Sh2,500 kwa mfuko wa kilo 50, kutoka Sh7,000 miaka mitatu iliyopita.

Serikali za kaunti sasa zinahusika katika mpango huo, na sera mpya inaundwa ili kuhifadhi mbolea katika mashamba ya kilimo ili kuwawezesha wakulima kupata bidhaa hiyo kwa urahisi.

Maeneo ya Bonde la Ufa na Magharibi mwa Kenya yanachukuliwa kuwa maneno makuu kwa uzalishaji wa nafaka nchini, lakini Kenya bado inakabiliwa na uhaba wa wastani wa tani 356,000 za mahindi kila mwaka, na hivyo kuilazimisha serikali kuagiza bidhaa hiyo kutoka nchi jirani.

Kaunti kuu zinazozalisha mahindi ni pamoja na Trans Nzoia, Uasin Gishu, Narok, Bungoma, Kakamega, Kericho, Bomet, Nandi, na Nakuru, ambazo kwa pamoja huchangia asilimia 50 ya uzalishaji wa mahindi kitaifa.

Lakini uzalishaji huo umetatizika kutokana na ugonjwa unaoathiri mahindi wa Lethal Necrosis (MLND) uliohasiri hasa kaunti za Bomet, Narok, na Kericho.

Licha ya kupungua kiasi kwa uzalishaji katika nchi jirani za Tanzania na Uganda, Kenya inatarajiwa kushuhudia ongezeko la asilimia 20 la uzalishaji wa mahindi mwaka huu, huku ardhi iliyopandwa mahindi ikiongezeka hadi hekta milioni 2.4 mwaka wa 2023 na ikitarajiwa kufikia hekta milioni 10.8 katika miaka mitano.

“Usajili wa wakulima kupitia njia ya kidijitali kwa ajili ya mpango wa utoaji wa mbolea ya ruzuku utafanywa endelevu na serikali.

“Hii itahakikisha kwamba hakuna mkulima anayeachwa nyuma katika mikakati inayolenga kufanya kilimo kuwa biashara kuu nchini,” akasema Dkt Ronoh.

Angaa wakulima 3,458,152 wamesajiliwa chini ya mfumo huo wa kielektroniki, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka. Dkt Douglas Kangi alibainisha kuwa kwa sasa kuna magunia 670,000 pekee ya hifadhi ya mahindi katika NCPB ambayo hayatoshi kudumu kwa matumizi.

“Kuna magunia milioni 35.2 ya kilo 50 ya mahindi ilhali magunia milioni 7.1 huhitajika kila mwezi kwa matumizi nchini,” Dkt Kangi alisema.