Habari za KitaifaMakala

Kwa nini Raila kujiapisha rais 2018 huenda kumnyime kiti cha AUC

Na JUSTUS OCHIENG September 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI Mkuu wa zamani Raila Odinga ameanza kampeni zake za kuwania kiti cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) kwa matumaini makuu, japo angali anakumbwa na viunzi kadhaa vinavyoweza kuzima nyota yake.

Mkutano wa Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliokamilika juzi ulitoa nafasi bora kwa Rais William Ruto kushawishi marais wenzake wa Afrika wamuunge Bw Odinga mkono.

Mkutano huo uliohudhuriwa na marais au viongozi 53 wa mataifa ya Afrika jijini Beijing, China, ulifanyika siku chache baada ya Serikali ya Kenya kumzindua rasmi Bw Odinga katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Nairobi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na marais watatu wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Lakini wataalamu wa masuala ya mahusiano ya kimataifa wanashauri kwamba serikali inapasa kujitahidi kurekebisha makosa yaliyochangia Kenya kukosa kushinda kiti hicho katika uchaguzi uliofanyika 2017.

Mkenya alishindwa awali

Waziri wa zamani wa Masuala ya Kigeni Amina Mohamed alishindwa na mwenyekiti wa AUC anayeondoka Moussa Faki Mahamat wa Chad, baada ya awamu saba ya upigaji kura.

Wataalamu wanataja hatua ya Rais wa Amerika kuitwika Kenya hadhi ya mshirika wake mkuu asiye mwanachama wa kundi la kujihami la NATO, suala la mataifa yanayozungumza Kifaransa kupiga kura pamoja, uwezekano wa kusalitiwa na nchi jirani wakati wa kura ya siri na suala la umri, kama visiki ambavyo Kenya inafaa kuzingatia kwa uzito.

Aidha, kuna wasiwasi kwamba hatua ya Bw Odinga “kujiapisha” mnamo 2018 kama “Rais wa Wananchi” na madai kuwa ana uhusiano wa karibu na viongozi kadhaa wa upinzani barani Afrika, inaweza kuwatia woga baadhi ya marais watakaoshiriki uchaguzi huo Februari 2025.

Wakati wa hafla ya kumzindua rasmi Bw Odinga katika Ikulu ya Nairobi mwezi jana, Rais wa Uganda Yoweri Museveni alidai baadhi ya washirika wa Odinga wanashirikiana na upinzani nchini mwake kuhujumu utawala wake.

Kulingana na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand Prof Gilbert Khadiagala, changamoto kubwa ya Kenya katika kinyang’anyiro cha AUC inahusiana na heshima yake.

“Kenya inaonenakana kama inayopendelea pande fulani katika siasa za ulimwengu. Juzi ilikubali hadhi ya kuwa mshirika mkuu wa Amerika asiye mwanachama wa NATO, hali ambayo imeshusha sana hadhi ya Kenya barani Afrika,” akasema.

“Heshima ya Kenya imeshuka haswa miongoni mwa nchini za Kusini mwa Afrika ambazo hupinga Amerika. Ukizingatia kwamba Amerika pia inachukiwa katik nchini za eneo la Sahel na Magharibi mwa Afrika, unaona ukweli kuhusu uwezekano wa Kenya kuonekana kuegemea Amerika utaathiri uchaguzi wa mwenyekiti wa AUC,” anasema Profesa Khadiagala.

Tafsiri: CHARLES WASONGA