Habari za Kitaifa

Magavana saba wanawake wamsukuma Waiguru apambane na Ruto 2027

Na PIUS MAUNDU, BENSON MATHEKA August 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru amehimizwa kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao, himizo ambalo alionekana kukubali.

Iwapo Bi Waiguru ataitikia wito huo na kugombea kiti hicho kikuu, hii itamaanisha kwamba atapingana na Rais ambaye wapo pamoja kwenye UDA kwa sasa.

Viongozi wanawake waliokutana Machakos kwa siku mbili walimshinikiza waziri huyo wa zamani kugombea urais baada ya kukamilisha muhula wake wa pili kama gavana.

Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani na aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu, walimpigia debe Bi Waiguru wakisema anatosha kuwa kiongozi wa nchi hii.

“Mungu ajibu maombi hayo,” Bi Waiguru alisema baada ya kauli za Bi Ngilu na Bi Achani.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Magavana alikuwa akiitikia mwito wa magavana hao wawili ambao walisema kwamba amedhihirisha kwamba ana chochote kinachohitajika kuongoza nchi kufikia ufanisi mkubwa.

“Tunataka kuona mmoja wa wanawake akiwa Rais wa Kenya. Amerika kwa sasa inaelekea kuwa na rais mwanamke. Na wanawake wa Kenya wana kile kinachohitajika kutoa rais. Waiguru, kwa kuwa umetimiza miaka kumi ya ugavana, ni kiti gani kingine kikubwa zaidi utakachowania. Usiulize ni kipi. Hakuna mtu mwingine mwenye uzoefu zaidi yako. Umekuwa gavana na waziri. Na kwa hivyo hupaswi kuogopa kusonga mbele kwa sababu una kile kinachohitajika,” Bi Ngilu alisema.

Bi Achani alimuunga mkono.

“Bi Waiguru ametuongoza vyema katika Baraza la Magavana. Umefanya kazi vizuri. Una sifa za kupanda ngazi nyingine ya uongozi. Kama wanawake tuna uwezo. Baada ya muhula wako wa ugavana kukamilika, kuza mwanamke mwingine kukurithi na uwanie nafasi kubwa ya uongozi,” Bi Achani aliongeza.

Viongozi hao walizungumza jana katika Mji wa Machakos, siku ya pili ya kongamano kuhusu uongozi wa wanawake ulioandaliwa na G7, chama cha  magavana wanawake katika Baraza la Magavana.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kajiado, Bi Leah Sankaire ambaye ni afisa mkuu katika bodi ya ushauri ya G7, alifichua kuwa magavana hao wanawake wanalenga nafasi ya naibu rais katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

“Tuna mkakati wa kuongeza idadi ya magavana wanawake kutoka 7 wa sasa hadi 24 katika Uchaguzi Mkuu wa 2027. Magavana wanawake ambao wanahudumu muhula wao wa kwanza wanapaswa kupewa fursa ya kukamilisha muhula wao wa pili. Wale ambao wamemaliza muhula wao wa pili wanapaswa kuruhusiwa kuwania nyadhifa za juu nchini Kenya. Kama wanawake wa Kenya tunasema nchi iko tayari kwa naibu rais mwanamke,” akasema.

Mke wa kiongozi wa Azimio Raila Odinga Ida Odinga na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka waliunga wito wa kuongeza idadi ya viongozi wanawake.

Bi Odinga alisema kuwa msukumo huo unapaswa kupanuliwa ili kujumuisha wabunge na wawakilishi wadi huku Bw Musyoka akitoa changamoto kwa wanawake ambao tayari wako katika uongozi kufanya kazi kwa bidii akisema juhudi za kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi zitakuwa rahisi wale walio katika nyadhifa za uongozi watakapotekeleza majukumu yao.

“Sina tatizo la kuwa na hata magavana 30 wanawake,” alisema.

Mkutano huo wa siku mbili ulikuwa sehemu ya mpango mpana  wa magavana wanawake katika  Baraza la Magavana kuonyesha mafanikio ya Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti. Ulihudhuriwa na  Bi Waiguru, Bi Achani na magavana Cecily Mbarire (Embu), Gladys Wanga (Homabay), Susan Kihika (Nakuru).