Habari za Kitaifa

Matarajio ya wenyeji Mlima Kenya Ruto akianza ziara wiki ijayo

Na WAANDISHI WETU March 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wa Mlima Kenya wameelezea yale wanayotarajia kutoka kwa Rais William Ruto kabla ya ziara ya maendeleo iliyopangwa kufanyika wiki ijayo.

Kukamilisha miradi kadhaa iliyokwama na kutekeleza ahadi mbalimbali alizotoa rais katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ni masuala yanayoongoza orodha iliyotajwa.

Rais Ruto anatarajiwa kuanza ziara Mlima Kenya Aprili 1, 2025 kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katika Kaunti ya Nyeri, wamiliki ardhi na wafanyabiashara kwenye barabara kuu ya Kenol – Marua wanatumai Rais Ruto atasuluhisha malipo ya mali yao ambayo yamecheleweshwa kwa karibu miaka minne.

“Nina nakala ya kupima thamani inayoashiria serikali inadaiwa na familia yangu Sh4 milioni. Malipo hayo ambayo bado hayajatekelezwa yameathiri mchakato wa urithi,” alisema mkazi, Michael Muriithi.

Wakazi Kirinyaga wametaja miradi chungu nzima iliyokwama iliyoanzishwa na Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta.

Mwenyekiti wa chama cha Jubilee (JP) Kirinyaga, Mureithi Kang’ara, alisema wanakandarasi walitelekeza barabara za Kutus-Kimbimbi – Kanjinji, Kiandegwa – Ng’othi – Kagio, Baricho – Getuya- Kiamaina, PI- Kiamutugu na Kianyaga – Thumaita.

Taasisi ya Utafiti kuhusu Matibabu (KEMRI) ya Sh15 bilioni, Mwea, imekwama na wanatarajia rais aifufue.

“Siasa zitafanyika 2027, tuna zaidi ya miaka miwili iliyosalia, tuzingatie miradi ya maendeleo na kuimarisha vijana, serikali ndiyo pekee iliyo na raslimali, rais apatiwe muda kuendeleza eneo,” alisema Bw Kang’ara.

Wakazi wanatumai rais atatimiza ahadi yake ya kuboresha mradi wa mpunga kupitia ujenzi wa mifereji.

Laikipia, wakazi wanatumai ziara ya rais itatimiza ahadi ya muda mrefu ya kuweka lami barabara ya Nanyuki-Rumuruti ya kilomita 80 ambayo imejadiliwa kwa karibu miongo minne.

Ni mara ya kwanza kwa Rais Ruto kuzuru eneo la Mlima Kenya kwa minajili ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo, hasa baada ya aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua kubanduliwa mamlakani.

Bw Gachagua, Mlima Kenya ikiwa ngome yake kisiasa, ‘amemkaribisha’ Ruto ila anamtaka aambie wakazi maendeleo aliyowafanyia.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, Dkt Ruto alipokea uungwaji mkono mkubwa, akizoa zaidi ya asilimia 40 ya kura zilizopigwa.