Habari za Kitaifa

Mchezo wa taon? Ruto atuma Riggy G mkutanoni licha ya ‘uhusiano baridi’


LICHA ya uhusiano wao kuonekana kuingia baridi, Rais William Ruto Jumatano alimtuma naibu wake Rigathi Gachagua kumwakilisha katika kongamano la kimataifa lililofanyika Nairobi.

Rais Ruto yuko Amerika kuhudhuria kongamano la Umoja wa Mataifa jijini New York na hivi majuzi, Bw Gachagua amekuwa akidai wabunge washirika wa kiongozi wa nchi wanapanga kuwasilisha hoja ya kumuondoa mamlakani.

Bw Gachagua alionekana kumhusisha rais na mipango hiyo ya kumtimua akisema ili hoja hiyo ifike bungeni, ni lazima iwe na baraka za kiongozi wa nchi.

Naibu Rais amekuwa akimuomba Rais amruhusu ahudumu kwa miaka mitatu iliyosalia ya muhula wa kwanza wa serikali ya Kenya Kwanza akilalamika kuwa, aliondolewa katika kundi la WhatsApp la kupanga shughuli za kiongozi wa nchi.

Lakini jana Jumatano, Bw Gachagua aliambia Kongamano la 41 la Kimataifa la Chama cha Bustani za Sayansi na Ubunifu Duniani lililofanyika Nairobi kwamba, alitumwa na Rais kumwakilisha.

Kwenye kongamano hilo, Bw Gachagua alitoa changamoto kwa nchi za Afrika kukumbatia teknolojia ya Akili Unde (AI) kama njia ya kuimarisha uchumi.

Alisema sekta mbalimbali nchini tayari zimekumbatia AI.

“Kwa niaba ya Rais William Ruto na wananchi wa Jamhuri ya Kenya, tunashukuru chama hiki kwa ubunifu huu maalum,” Bw Gachagua alisema.

“Nchi zinazoongoza hasa katika matumizi ya teknolojia duniani zinavuna kutokana na AI hasa katika sekta za kilimo, afya, biashara, viwanda, utalii, elimu, miongoni mwa sekta nyingine muhimu za uchumi. Kenya na Afrika haziwezi kufanikiwa kwa kutumia teknolojia na uvumbuzi kutoka nje pekee. Tuna rasilimali na changamoto za kipekee, ambazo lazima ziongoze uwekezaji wetu hasa katika utafiti na maendeleo,” alisema.

Siku chache zilizopita, seneta wa Tana River Danson Mungatana aliwasilisha hoja ya kumsuta Bw Gachagua katika bunge la Seneti.