Mchujo wazua hofu chama cha Gachagua madai ya upendeleo yakiibuka
Mvutano unaanza kutokota ndani ya chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, huku baadhi ya wanasiasa wanaotaka tiketi za chama hicho wakihofia kuwa viongozi fulani wanapendelewa kabla ya uchaguzi wa mchujo.
Wagombea hao wanadai kuwa licha ya kuahidiwa usawa kushindania tiketi, baadhi ya wapinzani wao wanaonekana kuwa na uungwaji mkono wa moja kwa moja kutoka kwa kiongozi wa chama na washirika wake wa karibu.
Hali hii inazua wasiwasi hasa katika eneo la Mlima Kenya, ambako DCP inajitahidi kuimarisha ushawishi wake huku ikipanua shughuli zake katika maeneo mengine ya nchi.
Mvutano huo unaripotiwa katika kaunti za Nyeri, Kirinyaga, Kiambu na Nakuru, ambako wanasiasa wanajiandaa kuwania viti vya ugavana, useneta, ubunge na uwakilishi wa wanawake katika uchaguzi wa 2027.
Baadhi ya wagombea wanahofia kuwa juhudi zao za kutafuta uungwaji mkono mashinani, kuchangia shughuli za chama na kujenga mitandao ya kisiasa huenda zisihesabiwe ikiwa tayari Gachagua ameamua nani anapaswa kupewa tiketi.
Aliyekuwa mbunge maalumu Maina Kamanda amedokeza kuwa DCP inaweza kuamua kuwaunga mkono wagombea fulani katika maeneo maalumu. Pia alionya kuwa Gachagua anaweza kuwakataa wanasiasa wanaohamia chama hicho kutoka kambi ya Rais William Ruto iwapo watashukiwa kuwa vibaraka wa serikali.
Kamanda alidai kuwa baadhi ya wanasiasa waliohama Ruto wamekuwa wakimfuata Gachagua na pesa wakitarajia kujipatia nafasi ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, alisema Gachagua hutumia rasilimali nyingi kuchunguza uwezo wa wagombea kabla ya kuwakubali, ili kuepuka kuwazawidi watu ambao wamepoteza umaarufu miongoni wwa wapigakura.
Gachagua amekuwa akisisitiza kuwa chama hicho kitafanya mchujo huru na wa haki.
“Wagombea wote wa DCP watashindana katika mchujo na washindi ndio watakaobeba bendera ya chama katika uchaguzi,” alisema alipohutubia mkutano wa kisiasa mjini Kagumo, Kaunti ya Kirinyaga.
Alisema hakuna mtu atakayepewa tiketi ya moja kwa moja bila kushindana na wengine. Alirudia ahadi hiyo katika mkutano mwingine Laikipia mwezi Agosti.
Hata hivyo, kauli hizo zimeibua maswali baada ya Gachagua kumuidhinisha hadharani Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango kuwania ugavana wa kaunti hiyo.
“Tuko na seneta wa Kirinyaga ambaye ndiye atakuwa gavava mwaka ujao wa kaunti ya Kirinyaga,” alisema kabla ya kumpa Murango kipaza sauti.
Hatua hiyo imewaacha baadhi ya wagombea wakijiuliza iwapo ahadi ya mchujo wa wazi itatekelezwa.
Mchanganuzi wa siasa Profesa Macharia Munene anasema mvutano huo unatokana kwa kiasi kikubwa na kukua kwa umaarufu wa DCP na wanasiasa wengi wanaotaka kujiunga na chama hicho.
“Chama kimekuwa maarufu kwa kiasi kikubwa, na sasa watu wanaotaka nyadhifa au wanaoamini kuwa njia pekee ya kufanikiwa kisiasa ni kuhusishwa nacho wanakikimbilia, hata kama hawakiamini,” alisema.
Anasema hali hiyo inawaweka katika nafasi ngumu wanachama waliochangia kukijenga chama hicho wakati hakikuwa na umaarufu mkubwa.
Baadhi ya waanzilishi na wafuasi wa awali wanahisi kuwa kujitolea kwao kunawapa haki ya kuwa na sauti kubwa katika maamuzi ya chama, hasa wakati wageni wanapoingia wakitafuta tiketi.
“Wamekijenga chama hadi kikawa maarufu. Kwa hivyo, wanahisi kuwa wao ndio wenye umiliki wake,” alisema Profesa Munene.
Hata hivyo, alionya kuwa wanachama wa muda mrefu wanapaswa kuwa waangalifu ili wasipoteze nafasi zao kwa wageni wanaoweza kuwa na nia ya kutumia umaarufu wa chama kujipatia madaraka.
Katika Kirinyaga, mbali na Murango, Gachagua anaripotiwa kumuunga mkono Njeri Maina kuwania uwakilishi wa wanawake na MCA wa Baragwi David Mathenge kuwania useneta.
Wanaowania nyadhifa hizo ni pamoja na Wangui Ngirici katika kinyang’anyiro cha ugavana na wakili Ndegwa Njiru katika kinyang’anyiro cha useneta.
Mvutano ulijitokeza wazi wakati wa ziara ya Gachagua katika kaunti hiyo Agosti 16, 2026, ambapo Kaimu Katibu Mkuu wa DCP John Methu alilazimika kuingilia kati kutuliza umati kufuatia hali ya kutoelewana kuhusu uwepo wa Ngirici.
Mwaniaji wa ubunge wa Gichugu Njeri Mbogo pia anaripotiwa kuadhibiwa na chama baada ya kulalamika hadharani kuwa hakuruhusiwa kuhutubia wafuasi wakati wa ziara hiyo.
Malalamishi mengine yanahusu uteuzi wa viongozi wa matawi ya chama, huku baadhi ya wagombea wakidai kuwa makundi fulani yanapendelewa. Wengine wanasema wanachangia maandalizi ya mikutano ya Gachagua lakini wapinzani wao wanapewa nafasi zaidi ya kuonekana na kuhutubia wafuasi.
Mvutano huo unaweza kuwa fursa kwa vyama vingine vinavyotafuta kupanua ushawishi wao Mlima Kenya.
Chama cha People’s Party of Kenya kinachoongozwa na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, pamoja na People’s Liberation Party cha aliyekuwa Waziri wa Sheria Martha Karua, vinaweza kuvutia wagombea watakaokosa nafasi ndani ya DCP.
Kwa mujibu wa Profesa Munene, wanasiasa wanaoamini kuwa wana uungwaji mkono wa kutosha wanaweza kuamua kuwania viti kupitia vyama vingine iwapo watanyimwa tiketi wanazotaka.
“Kwa sababu mtu akiwa maarufu na akahisi chama kinamdhulumu, anaweza kuwania kupitia chama kingine na akashinda,” alisema.
Kwa Gachagua, changamoto ni kusawazisha maslahi ya wanachama wa zamani na wanasiasa wapya wanaoingia chamani. Kuwapendelea washirika wa karibu kunaweza kuwakatisha tamaa wagombea wengine, huku kuwapa wageni nafasi nyingi kukiwa na hatari ya kuwakasirisha waliochangia kukijenga chama.
DCP inakabiliwa na mtihani wa kuonyesha kuwa umaarufu wake hautategemea tu jina la kiongozi wake, bali pia uwezo wa kuwapa wanachama nafasi sawa ya kushindania uongozi.