Habari za Kitaifa

Mishahara ya mawaziri, magavana, wabunge kuongezwa mwezi huu raia wakilia

Na EDWIN MUTAI July 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HUKU vijana wanaoandamana wakitaka mishahara ya wabunge ipunguzwe, walipaji ushuru wataumia zaidi huku mishahara ya Mawaziri, Wabunge, Magavana, madiwani na afisi zingine kuu za Serikali ikitarajiwa kuongezwa mwezi huu.

Ni mshahara wa Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua, wanaopata Sh1,443,750 na Sh1,227,188 mtawalia, ambayo haitarekebishwa katika mwaka wa kifedha ulioanza Jumatatu Julai 1, 2024.

Nyongeza ya mishahara hiyo ni kwa mujibu wa notisi ya gazeti la serikali iliyochapishwa na Tume ya Mishahara (SRC) mnamo Agosti 9, 2023.

Kupitia notisi hiyo, SRC iliweka mshahara na marupurupu ya Maafisa wa Serikali kwa miaka ya fedha 2021/2022–2024/2025.

“Muundo wa Mishahara ya Kila Mwezi kwa Maafisa wa Serikali ya Kitaifa kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2024/2025, kuanzia tarehe Julai , 2024,” SRC ilisema kwenye notisi hiyo.

Hata hivyo, mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich alisema nyongeza ya mishahara iliyopendekezwa kwenye notisi ya gazeti la serikali ya Agosti 9, 2023 haijatekelezwa.

“Inategemea upatikanaji wa fedha na uendelevu wa kifedha,” Bi Mengich alisema akijibu swali la Taifa Leo.

Iwapo notisi hiyo itatekelezwa, mishahara ya Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi, Mawaziri 22, Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei na Katibu wa Baraza la Mawaziri Mercy Wanjau itafikia Sh990,000 kila mmoja kutoka Sh957. 000.

Wabunge na Maseneta, ambao mshahara wa sasa ni Sh725,502 utaongezwa hadi Sh739,600 kila mwezi.

Mshahara wa magavana umerekebishwa kutoka Sh957,000 hadi Sh990,000 huku ule wa MCA ukiongezeka kutoka Sh154,481 hadi Sh164,588 kila mwezi.

Nyongeza hiyo mpya ya mishahara inajiri wakati Rais William Ruto anakabiliwa na maandamano ya umma ili kupunguza matumizi ya pesa na kupunguza mzigo wa ushuru kwa raia wa kawaida.

Katika hotuba yake kwa taifa kufuatia maandamano ya Generation Z, Rais alielekeza kupunguzwa kwa bajeti ya matumizi yasiyo ya lazima katika ofisi yake, ikiwa ni pamoja na usafiri, ukarimu na ununuzi wa magari kuziba pengo la Sh346 bilioni lililosababishwa na kukataliwa kwa Mswada wa Sheria ya Fedha wa 2024.

Chini ya muundo huo mpya, mishahara wa maspika wa Bunge la Kitaifa na Seneti ambao kwa sasa wanapata Sh1,185,327 utapanda hadi Sh1,208,362 huku ule wa Manaibu Spika wa Mabunge yote mawili ukifikia Sh966,690, kutoka Sh948,261.

Kando na mishahara yao mikubwa, Wabunge na Maseneta hulipwa marupurupu ya kuhudhuria vikao vya Kamati huku wenyeviti wakipata Sh15,000 kwa kila kikao hadi kima cha juu cha Sh240,000 kwa mwezi.

Makamu mwenyekiti hupata Sh12,000 kwa kikao hadi Sh192,000 kwa mwezi huku wanachama wakipata Sh7,500 kwa kikao hadi Sh120,000 kwa mwezi.

Mishahara ya Makatibu Wakuu 51, Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi, Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi sasa itapanda kutoka Sh792,519 walizopata mwezi uliopita hadi Sh819,844 mwishoni mwa mwezi huu.

Mshahara mpya wa Naibu Inspekta-Jenerali, Huduma ya Polisi ya Kenya, Naibu Inspekta-Mkuu, Utawala na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai utakuwa Sh684,233 kutoka Sh652,742 za sasa.

Katika kaunti, mshahara wa Gavana wa Kaunti umerekebishwa kutoka Sh957,000 hadi Sh990,000 huku ile ya Naibu Gavana wa Kaunti ikipanda kutoka Sh652,742 hadi Sh684,233.

Mshahara wa waziri wa kaunti utaongezeka kutoka Sh413,079 hadi Sh422,526 huku ule wa Spika wa Bunge la Kaunti ukirekebishwa kutoka Sh537,003 hadi Sh549,283.

Naibu Spika atapokea Sh247,943 kutoka Sh231,722 huku Kiongozi wa Wengi/Wachache anayepata Sh191,324 akipata Sh204,717.

MCA anayepokea Sh154,481 sasa ataweka mfukoni Sh164,588 kila mwezi.