Habari za Kitaifa

Mtihani kwa Ogamba, KNUT, KUPPET zikitangaza mgomo wa walimu

Na DAVID MUCHUNGUH August 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI mpya wa Elimu Migos Ogamba anakabiliwa na kibarua kigumu huku miungano ya walimu nchini ikitangaza kuwa walimu watashiriki mgomo na kulemaza shughuli za elimu katika muhula wa tatu.

Bw Ogamba aliapishwa katika Ikulu ya Nairobi Alhamisi, Agosti 8, 2024 na anachukua usukani kwenye wizara ambayo tayari inakabiliwa na changamoto si haba.

Uongozi wa Chama cha Kutetea Walimu Nchini (KNUT) na ule wa Muugano wa Walimu Wakuu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET) umetangaza kuwa walimu watashiri mgomo wakati shule zitakuwa zikifunguliwa kwa muhula wa tatu mwishoni mwa mwezi huu, Agosti.

Alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa iliyokuwa ikiwapiga mawaziri msasa, Bw Ogamba alisema alifahamu changamoto ambazo zilikuwa zikiathiri sekta hiyo.

Alitaja uhaba wa walimu, kukosekana kwa miundomsingi katika shule mbalimbali na wazazi kutohusishwa kwenye usimamizi wa shule kama baadhi ya changamoto ambazo zilikuwa zikiathiri sekta hiyo.

Iwapo mgomo wa walimu utafanyika muhula wa tatu basi watahiniwa wa mtihani wa gredi ya sita na wale wa kidato cha nne, watataabika kwenye maandalizi yao ya kukabili mitihani hiyo.

Baadhi ya matakwa ambayo yameibuliwa na walimu yanastahili kusuluhishwa na Tume ya Kuwaajiri Walimu Nchini (TSC).

Hata hivyo, Bw Ogamba ana kibarua cha kuzuia mgomo huo na hata itamlazimu kujifunza jinsi watangulizi wake walikuwa wakishughulikia utata huo.

Wanafunzi, wazazi, walimu pamoja na washikadau wengine wanasubiri kuona jinsi Bw Ogamba atashughulikia wanafunzi kujiunga na gredi ya tisa ambayo kupitia Mtaala wa Utendaji na Umilisi (CBC) ndio wa mwisho kwenye masomo ya shule ya msingi.

“Nitabadilisha tu sera ambazo hazifanyi kazi kwa sababu serikali ni ile ile,” akasema Bw Ogamba.

Waziri huyo alichukua hatamu za wizara yake Jumatatu, Agosti 12, 2024 lakini mtangulizi wake Ezekiel Machogu hakuwepo kumkabidhi afisi hiyo rasmi.

Bw Ogamba alikuwa mgombeaji mwenza wa Bw Machogu kwenye mbio za kusaka ugavana wa Kisii mnamo 2022.

Imetafsiriwa na Cecil Odongo