Pigo kwa Ruto jopo la Maraga kuboresha idara ya polisi likiharamishwa
RAIS William Ruto Alhamisi, Aprili 10, 2025 alipata pigo kwenye jitihada zake za kufanikisha mageuzi katika idara ya usalama baada ya jopo alilounda kuharamishwa na mahakama.
Jopo hilo lililoundwa Desemba 2022, lilikuwa likiongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga.
Mageuzi katika idara hiyo yalilenga kuhakikisha maslahi ya polisi na maafisa wa magereza yanaimarishwa.
Maafisa hao walikuwa waongezwe mishahara, kuwe na mfumo unaoeleweka kuwapandisha ngazi na kuimarishwa kwa makazi yao ambayo yako katika hali mbaya.
Wizara ya Usalama ilisema kuwa mageuzi hayo yangegharimu Sh108 bilioni kufanikisha utekelezaji wake.
Kuharamishwa kwa jopo hilo pia kunatarajiwa kuathiri ujenzi wa makazi 28,000 ya polisi wa magereza na kuimarishwa kwa mazingira yao ya kazi.
Alhamisi, Jaji Lawrence Mugambi alisema kubuniwa kwa jopo hilo na kuweka majukumu yake chini ya Tume ya Kitaifa ya Huduma kwa Polisi (NPSC) ilikuwa kinyume cha Katiba.
Kwa mujibu wa jaji huyo, majukumu ambayo yalitekelezwa na jopo la Bw Maraga ni jukumu la NPSC na hayo yamewekwa wazi kwenye Katiba.
“Mapendekezo yoyote ambayo yalitokana na jopo hilo ni haramu, hayafai kutekelezwa na yanaenda kinyume cha Katiba,” akasema Jaji Mugambi.
“Kwa kuipa jopo hilo majukumu ambayo yanafahamika kama ya NPSC kwenye Katiba, hatua ya Rais ilikiuka Katiba. Rais hafai kutumia mamlaka yake chini ya Katiba, kutoa majukumu ya tume huru kama NPSC kwa mtu yeyote au jopo,” akaongeza.
Jaji huyo aliendelea na kusema hatua ya rais ilikiuka msingi wa utawala wa kisheria na hana mamlaka kuingilia majukumu ya asasi huru za kikatiba.
Wizara ya Usalama wa Ndani ilikuwa imeanzisha utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti hiyo, miongoni mwao kupandishwa kwa mishahara ya polisi, askari wa magereza na wale wanaohudumu kwenye Huduma ya Polisi kwa Taifa (NPS).
Mapema mwaka huu, 2025, maafisa hao walipokea nyongeza ya asilimia 10 kutokana na kutekelezwa na kuzingatiwa kwa mageuzi ya jopo la Bw Maraga.
Desemba 2025, Rais alitangaza kuwa mpango wa kujenga makazi bora kwa maafisa wa magereza ungeanza mara moja.
Wizara ya Usalama wa Ndani nayo Septemba iliteua Kamati Kuu kusimamia utekelezaji wa mageuzi hayo.
Jopo la Bw Maraga lilibuniwa Desemba 2022 kama sehemu ya kutekelezwa kwa ahadi ambazo zilitolewa na Rais Ruto kabla ya kuchaguliwa kwake.
Alitoa ahadi ya kuipa hadhi idara ya polisi ajenda ambayo hata ilikuwa kwenye manifesto yake.
Kesi hiyo iliwasilishwa na wakili na mwanaharakati Dkt Magare Gikenyi ambaye alisema jopo hilo liliingilia majukumu ya NPSC.
Mahakama, hata hivyo, ilisema jopo lenyewe lingejihusisha na kuibuka na mpango wa kushauri serikali kuhusu utekelezaji wa masuala ya kuimarisha maslahi ya maafisa hao wa usalama lakini kupitia NPSC.