Habari za Kitaifa

Raila ametengewa wizara tano japo asisitiza Kalonzo, Karua na Kioni wakubali kwanza – Ripoti

Na JUSTUS OCHIENG July 21st, 2024 2 min read

MAELEZO kuhusu wizara ambazo Rais William Ruto ametengea kiongozi wa ODM Raila Odinga katika baraza lake la mawaziri yamefichuka, huku kukiwa na mzozo katika upinzani kuhusu ukuruba wake na serikali ya Kenya Kwanza.

Taifa Jumapili imebaini kuwa hali katika kambi ya Bw Odinga ndio ilisababisha kucheleweshwa kwa majina ya wandani wake kuteuliwa katika baraza la mawaziri Rais Ruto alipojaza nafasi 11 Ijumaa.

Rais Ruto amempa kinara wa upinzani angalau nafasi tano katika Baraza la Mawaziri, akitarajia kuwa na watu ambao watamsaidia katika kuleta mabadiliko nchini.

Wizara ambazo Bw Odinga alitengewa na ambazo hazijajazwa ni pamoja na Hazina ya Kitaifa na Mipango, Utumishi wa Umma, Madini na Uchumi wa Baharini na Masuala ya Bahari na Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda.

“Ruto anatoa wizara hizi, lakini Raila anasisitiza kwamba hapaswi kuzichukua ikiwa Kalonzo (Musyoka), (Martha) Karua na (Jeremiah) Kioni hawatakubali,” mwandani wa Bw Odinga aliambia Taifa Jumapili.

“Lazima tusema ukweli. Wizara ya Fedha inahusu wizara zote na ina mwakilishi katika kila bodi. Uchumi wa Baharini ndio uti wa mgogo wa kaunti za ODM kutoka Pwani hadi Busia hadi Turkana hadi Nyanza. Tunataka nini?”

Lakini huku Odinga akivutana na washirika wake katika Azimio la Umoja One Kenya, akiwemo aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyekiti wa baraza la muungano huo, mrengo wa Bw Musyoka umejitenga na hatua ya kiongozi huyo wa ODM kushirikiana na utawala wa Kenya Kwanza, ukisisitiza kuwa chama tanzu chochote kitakachokubali kitafanya hivyo kivyake na sio kama Azimio.

“Hatutashiriki au kuunga mkono mapendekezo ya serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Kenya Kwanza. Huu ni usaliti wa watu wa Kenya, hasa Gen Z na milenia, ambao wamekufa ili kuondoa nchi hii kutoka kwa utawala mbaya wa Kenya Kwanza, ushuru dhalimu, ufisadi, ukabila, ukosefu wa ajira, na. gharama ya juu ya maisha,” akasema Bw Musyoka kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Ijumaa.

“Hatutajiunga kwa sababu ya moja kwa moja kwamba vitendo hivyo ni usaliti wa maadili na kanuni za chama chetu cha muungano na vyama vyetu. Maadamu utawala wa Kenya Kwanza unaendelea kuwepo, hakuna kitakachobadilika. Kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri ni kujifanya tu.”

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alikosoa kurejeshwa kwa mawaziri sita katika Baraza la Mawaziri, na hivyo kuongeza mkanganyiko katika juhudi za Bw Odinga kushirikiana na serikali.

Mawaziri hao sita wa zamani Prof Kithure Kindiki (Masuala ya Ndani), Aden Duale ( Ulinzi), Alice Wahome (Ardhi), Soipan Tuya (Mazingira) na David Chirchir (Barabara) huku aliyekuwa waziri wa Biashara Rebecca Miano akitajwa kuwa Mwanasheria Mkuu.

“Ni jambo la kutamausha sana. Itakuwa vigumu kwa mfano kuwa na mazungumzo ya ukweli kuhusu mageuzi na uwajibikaji katika sekta ya usalama na watu kama Duale na Kindiki wakiwa kwenye Baraza la Mawaziri. Wawili hao ni sehemu ya tatizo,” Bw Sifuna aliambia Taifa Jumapili.

Bw Odinga anasemekana kuwa katika hali ya kutatanisha iwapo atawasilisha orodha yake kwa Rais huku kukiwa na mvutano mkali kuhusu kurejea kwa mawaziri hao wa zamani.

Mshirika wake wa karibu aliambia Taifa Jumapili kwamba kumekuwa na majaribio kadhaa, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa kaka yake Dkt Oburu Oginga, kukubali ombi la Dkt Ruto.

“Lakini kufikia jioni ya leo (Jumamosi), yeye (Bw Odinga) bado alikuwa akiwasiliana na Kalonzo,” alisema.